Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John pombe Magufuli amesema Afrika inakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na nchi za Nordic kabla na baada ya harakati za ukombozi.
Ameyasema hayo leo, Novemba 8, 2019, alipo hutubia mkutano wa 18 wa mawaziri wa mabo ya nje wa Afrika na Nordic uliofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Amesema nchi hizo zimechangia katika kuendeleza na kuinua huduma za kijamii na kiuchumi kama vile afya, elimu, kilimo, sayansi na taknolojia, nishati, mazingira pamoja na kulinda amani na usalama.
Ametolea mfano nchi ya Tanzania ambayo nchi za Nordic zimechangia ujenzi wa kituo cha Elimu kibaha, chuo cha utafiti wa kilimo Uyole, vyuo mbalimbali vya ufundi na kampeni za kufuta ujinga katika miaka ya 70.
Akizungumza katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na mawaziri 29 wa nchi za Afrika, na mawaziri 5 wa nchi za Nordic ambazo ni Norway, Swedan, Denmark, Finland na Iceland amezishukuru nchi hizo kwa ushirikiano wake mzuri na nchi za Afrika.
Hata hivyo Rais Magufuli amesema kuna haja ya kubadilisha mwelekeo na kuingia katika mwelekeo wa kisasa unaojikita katika ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji.
Amesisitiza kuwa nchi za Nordic zenye watu wapatao milioni 27 zina uchumi mkubwa unaofikia pato la mwaka la dola za Marekani Trilioni 1.7 ikilinganishwa na nchi za Afrika zenye watu Bilioni 1.2 na pato lake la mwaka ni Trilioni 2.334 hivyo Afrika inapaswa kujifunza kutoka nchi za Nordic.
Aidha amebainisha kuwa Afrika ina eneo kubwa, asilimia 30 ya eneo lote duniani linalofaa kwa kilimo lipo Afrika, ukanda wa pwani ya bahari wenye urefu wa kilometa 30,500, mifugo, misitu, wanayamapori, mafuta, gesi, utalii na uchumi wake unakua vizuri kwa wastani wa asilimia 4.1.