Rais John Pombe Magufuli amelituma Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujenga ukuta wa kuzunguka vitalu vyenye madini ya Tanzanite katika eneo la Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ili kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo.
“Lile eneo la kitalu kuanzia A hadi D ambalo ndio lina mali nyingi ya Tanzanite, naagiza Jeshi la Wananchi kupitia Suma-JKT na wengine, najua wameshamaliza utafiti, waanze kujenga ukuta eneo hilo lote na kazi hii ifanyike haraka’’ amesema Magufuli.
Hata hivyo amefafanua kuwa ukuta huo utawekwa kamera na kutakuwa na mlango mmoja utakaowekwa vifaa maalumu vya kudhibiti biashara ya madini ya Tanzanite.
Ameongezea kuwa , ‘nataka niwaeleze ukweli ndugu zangu wa Simanjiro hata kama utameza Tanzanite utaonekana’’.
Pia ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kushiriki katika ununuzi wa Tanzanite.
Aidha, Rais Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa kukabiliana na wizi wa madini ya Tanzanite na ameitaka kamati inayoongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba John Kabudi kuanza kufanyia kazi taarifa zilizotolewa na wananchi kuhusu uchimbaji na biashara ya madini hayo ili mchakato wa kurekebisha mikataba ufanyike.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo kwenye sherehe ya ufunguzi wa barabara ya Kia – Mererani iliyofanyika katika eneo la Mererani.