Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge, abadilike na kuachana na upole badala yake awe mkali kwa lengo la kuhakikisha miradi ya jiji hilo inaenda vizuri.
Magufuli amesema hayo hii leo Oktoba 8, 2020, wakati akizungumza na wakazi wa jiji la jijini Dar es Salaam kwenye zoezi la kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani kilichopo maeneo ya Mbezi Mwisho.
“Ninajua mkuu wa mkoa wewe ni mgeni hapa lakini badilika uwe mkali usiwe sheikh au Askofu, ni lazima watu watimize wajibu wao, muondoe ‘damage’ ambayo iko kwenye mkataba,” amesema Magufuli.
Katika hatua nyingine rais Magufuli amewaomba wananchi wa jiji hilo kuwachagua wabunge na madiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.
“Japo leo siyo siku ya kampeni, nitashangaa sana wabunge wangu na madiwani wangu kama hawatochaguliwa kwa kazi nzuri zinazofanywa DSM, siwezi nikaondoka hapa bila kuwaombea kura, na Rais wa Malawi amekuja kunitembelea kwa sababu anajua nitashinda”amesema Magufuli.