Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
Rais Magufuli ameyasema hayo katika ziara yake Mkoani Pwani, wakati akizungumza na wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja, ikiwa ni ziara yake katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
“Najua mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa, sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa, ni lazima tufanye kazi, sasa hivi mvua zinanyesha limeni mazao ya chakula” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na pia amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Hata hivyo, Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo na ameahidi kutoa Shilingi Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga