Serikali ya Tanzania kupitia Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amesema hawaitaji kuendelea kupata aibu ambazo zimezoeleka za jalada kupotea au halionekani, au hadithi ya jalada linahitaji kufutwa vumbi kwanza katika kuendesha kesi ndani ya Mahakama zilipo nchini kwani sasa wanakuja na mfumo mpya wa tehama utakaoutumika kuhifadhi jalada mbalimbali.
Ameeleza hayo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya 22 ya siku ya Sheria na uzinduzi wa mwaka mpya wa kimahakama yaliyofanyika jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akiwa Rais John Magufuli na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi.
“Mahakama imejiwekea malengo ya kuongeza uwazi na ufanisi katika masuala ya utawala na uendeshaji wa mashauri na tehama tumeona ndio jibu sahihi kwa Mahakama karne ya 21 inayolenga kuwa na uwazi pamoja na ufanisi.
Mahakama hatuhitaji tena aibu za stakabadhi ya malipo ya shughuli haionekani, hatutaki kusikia mteja shauli lake liko wapi, kwa nani na ni lini au lipo mbele ya Jaji yupi”, amesema Profesa Ibrahimu Juma.
Pamoja na hayo, Jaji Mkuu amendelea kwa kusema “tumepanga kufuta hayo yote ili kujenga historia mpya katika msingi wa tehama, tumeadhimia na hatutaki kubaki nyuma na tutaendelea na kasi ya mabadiliko ya kunufaika kutokana na mafanikio makubwa ya tehama tumelenga kuyashuhudia na kunufaika kwenye eneo la usimamizi wa fedha, ukosaji wa takwimu, mapato, usikilizaji wa mashauri.
Kwa upande mwingine, Profesa Ibrahimu Juma amemkumbusha Rais Magufuli lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha Mahakama zinazotembea ili kuweza kuwafikia watu popote walipo.