Mahakama ya rufani imetupilia mbali rufaa ya Serikali, iliyokuwa ikipinga hukumu ya Mahakama kuu iliyobatilisha vifungu vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Oktoba 23, 2019 baada ya Mahakama hiyo ya rufani kukubaliana na hoja za jopo la mawakili lililoongozwa na Mpale Mpoki, Jebra Kambole ambaye alishinda kesi ya msingi, Alex Mgongolwa na Fulgence Massawe.
Akisoma hukumu hiyo, naibu msajili, Fussi amesema kuwa Mahakama kuu ilikuwa sahihi kuamua kuwa vifungu hivyo ni vya kibaguzi kati ya mtoto wa kike na wa kiume na havina manufaa kwa mtoto wa kike.
” Hivyo tunaitupilia mbali rufaa hii yote kutokana na kutokuwa na mashiko” amesema Fussi akinukuu hukumu hiyo.
Serikali ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyotokana na kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanaharakati na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi.
Akizungumzia hukumu hiyo Gyumi amesema ni ushindi muhimu kwa watoto wa kike nchini na kwamba majaji wamesimamia ukweli kwa ujasiri mkubwa, na kuahidi kuendelea kuelimisha jamii kuhusu hukumu hiyo na madhara ya ndoa za utotoni.
“Hukumu hii imewapa wasichana wa Tanzania ulinzi wa kisheria waliokuwa wakiukosa kilichobaki sasa ni kuhakikisha hukumu hiyo inatekelezeka haraka ndani ya mwaka mmoja kama ilivyoamriwa tangu awali na Mahakama kuu” Amesema Rebeca.
Pia amesema watakaa kujadiliana na kamati za Bunge zenye dhamana na masuala ya sheria kuhakikisha serikali inawasilisha bungeni haraka muswada wa marekebisho ya sheria hiyo.
Ikumbukwe kuwa katika kesi ya msingi namba 5 ya mwaka 2016, Rebeca alipinga vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa kwa kudai vinakiuka haki ya mtoto wa kike kupata elimu.