Mahakama ya Rufani Tanzania imewaachia huru watu wanne waliokuwa wanatumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja na kulipa faini ya jumla ya Sh. 20 milioni kwa kukutwa na kilo tano za nyama ya kiboko.
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Shaban Lila, Jaji Rehema Mkuye na Jaji Ignus Kitus walitoa uamuzi wao, wote wakiwaachia huru Matheo Ngua, Richard Masala, Jofrey Saimoni na Edwin Gerard.
Wanne hao walikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yao na Mahakama ya Wilaya ya Chunya na baadaye kupitishwa tena na Mahakama Kuu.
Majaji hao waliwaachia huru wakieleza kuwa Mahakama ya Wilaya ya Chunya haikuwa na Mamlaka ya kutoa hukumu hiyo kwakuwa hawakuwa na Hati maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Walieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, kesi za makosa ya uhujumu uchumi zinapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu, na kwamba ili Mahakama za chini ziweze kusikiliza ni lazima zipewe kibali maalum kinachoambatana na hati kutoka kwa DPP.
“Kwa Mamlaka tuliyopewa na Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa Kifungu cha 4(2) tunaamuru wakata rufaa waachiwe haraka, isipokuwa tu kama kuna sababu nyingine za kisheria,” Jopo la Majaji limeeleza.
Pamoja na mambo mengine, Jopo la Majaji lilieleza kuwa hakukuwa na ushahidi usio na shaka unaoweza kuwatia hatiani wakata rufaa.
Hukumu hiyo ilieleza kuwa nyama za kiboko walizodaiwa kukutwa nazo wakata rufaa ziliharibiwa lakini watuhumiwa hawakupewa nafasi ya kushuhudia jinsi ambavyo nyama hizo zilivyoharibiwa, hali iliyosababisha kuwe na shaka katika ‘kizibiti’ hicho.
Mahakama ilikubaliana na utetezi wa wakata rufaa kuwa walikutwa wakiwa wanavua kando ya Ziwa Rukwa, maelezo yaliyokubaliwa pia na shahidi aliyeletwa na upande wa mashtaka ambaye alisema walikutwa na nyavu za kuvulia samaki. Lakini Mahakama ya Wilaya ya Chunya na Mahakama Kuu zikawakuta na hatia ya kukutwa na Nyara za Serikali kinyume cha sheria.
Katika kesi ya msingi, ilielezwa kuwa watu hao pamoja na watu wengine ambao waliachiwa katika mchakato wa kesi kwenye Mahakama za chini, Septemba 6, 2015 walikutwa na kilo tano za nyama ya kiboko yenye thamani ya 3,990,000/-, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, katika tarehe tajwa, walinzi wawili wa Hifadhi ya Taifa ya Piti au kwa jina lingine Lutwati walikuwa waliokuwa kazini, waliona nyayo za binadamu katika eneo hilo.
Waliamua kuzifuatilia nyayo hizo hadi katika eneo ambalo walikuta kuna jiko la mkaa la kuchomea nyama. Karibu na eneo hilo pia kulikuwa na nyama ya myama aliyechinjwa ambaye walimtambua kuwa ni kiboko. Hata hivyo, hakukuwa na watu katika eneo hilo.
Ilielezwa kuwa baada ya kuangalia vizuri, walinzi hao waliona boti ikiwa Ziwani na ndani yake kulikuwa na watu. Waliifuata boti ile kwa kutumia boti yao ya kazi (patrol boat), baada ya kuhisi kuwa boti hiyo inauhusiano na kiboko aliyeuawa waliyemuona muda mfupi uliopita.
Walieleza kuwa kulikuwa na watu takribani saba kwenye boti ile, ambayo baada ya kuikamata walikuta kuna kilo tano za nyama ya kiboko. Ilielezwa kuwa watu hao pia walikutwa na bunduki ambayo waliitupa ndani ya maji ili kupoteza ushahidi. Walikamatwa na kufikishwa mahakamani, na wote walikana tuhuma hizo dhidi yao. Wengine waliachiwa katika mchakato wa kesi kwenye mahakama za chini na wanne walikutwa na hatia.
Kwa upande wa utetezi, watu hao wanne, waliiambia Mahakama kuwa walikutwa wakiwa wanavua pembezoni mwa Ziwa Rukwa, karibu na eneo la hifadhi na kwamba askari wa hifadhi waliwabambikizia nyama za kiboko.
Mahakama ya Wilaya ya Chunya ilisikiliza maelezo ya pande zote mbili na kuwatia hatiani watu hao wanne. Iliamuru wafungwe jela miaka 20 kila mmoja na kulipa faini ya jumla ya Sh. 20 milioni. Baadaye, Mahakama Kuu pia iliridhia uamuzi wa Mahakama ya Wilaya.
Watu hao waliamua kukata rufaaa kwenye Mahakama ya Rufaa, ambapo wamefanikiwa na kuachiwa huru.
Kupambana na corona: Ndege ya WFP kutua Dar leo na wafanyakazi
Kim Jong Un ashtukia usalama? Awatumbua Mkuu wa Intelijensia na wa Ulinzi wake