Hatimaye kitendaiwili cha sakata la Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad afike mbele ya Kamati ya Bunge kimeanza kutenguliwa kwa vitendo leo.
CAG ameitikia wito huo na tayari ameanza kuhojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge jijini Dodoma.
Kamati hiyo inamhoji CAG kufutia kauli aliyoitoa alipozungumza na chombo cha habari cha Umoja wa Mataifa, ambapo alieleza kuwa kama ripoti zake hazifanyiwi kazi na Bunge huo ni “udhaifu wa Bunge.”
Kauli hiyo ililaaniwa vikali na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alimtaka kufika mbele ya Kamati leo akionya kuwa endapo hataitikia wito huo atapelekwa kwa pingu.
Aidha, CAG alizungumzia wito huo baada ya mjadala mrefu na kueleza kuwa ana nia ya kuitikia wito, lakini alisisitiza kuwa maneno ‘udhaifu’ na ‘upungufu’ ni lugha ya kawaida ya kikaguzi.
Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu nchini leo imeisajili kesi iliyofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akiitaka Mahakama kutoa tafsiri ya Ibara ya 143(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Mamlaka ya CAG.
“Kumekuchaaaa! Kesi ya Zitto v. Job imekubaliwa kusajiliwa na Mahakama Kuu. Nimepata message sasa hivi,” ametweet Fatma Karume ambaye ni mwanasheria wa Zitto katika kesi hiyo.
Awali, Msajili wa Mahakama Kuu aliandika barua akikataa kusajili kesi hiyo kutokana na sababu mbili za taratibu za kisheria ambazo alizieleza, sababu ambazo Zitto na Fatma walizipinga vikali.
Hata hivyo, Jaji Mkuu aliwaeleza kuwa amemuandikia barua Jaji Kiongozi kufuatilia suala hilo, ambalo leo limekuwa na habari njema kwa wawili hao.
Nia ya Zitto ya kufungua shauri hilo, pamoja na mambo mengine ilitokana na kutokubaliana na wito wa Spika Ndugai kwa CAG, akieleza kuwa Spika hana mamlaka ya kuchukua hatua hiyo.