Mahakama nchini Marekani leo imemfutia muigizaji nyota wa ‘Empire’, Jussie Smollet, mashtaka yote ya jinai yaliyokuwa yanamkabili.
Mwanasheria wa Jussie, Tina Glandian ametangaza uamuzi huo wa Mahakama ambapo amedai kuwa mashtaka dhidi ya mteja wake ya kutoa taarifa za uongo kwa jeshi la polisi kuhusu kupigwa na watu wawili ambao walimtishia kwa kumpa maneno ya kiubaguzi wa rangi pamoja na masuala ya ushoga, yamefutwa rasmi.
Jussie alidai kuwa Januari 29 usiku, watu hao walimvamia mitaani na kumfunga kamba shingoni na kunyanyasa kwa muda huku wakitumia misemo ya watu wanaomuunga mkono Rais wa Marekani, Donald Trump.
Lakini uchunguzi wa awali wa polisi ulieleza kuwa Jussie alidanganya na kwamba aliandaa tukio hilo yeye mwenyewe na kuwalipa watu hao wawili ili kutekeleza azma yake baada ya kutoridhishwa na mshahara anaolipwa kwa kuigiza ndani ya ‘Empire’.
Waandaaji wa Empire walichukua hatua za haraka na kumfuta kazi kwa madai ya kuichafulia taswira kwa kuudanganya umma.
“Leo mashtaka yote ya jinai yanayomkabili Jussie Smollet yamefutwa na rekodi ya maisha yake imesafishwa rasmi. Jussie alishambuliwa na watu wawili ambao hakuweza kuwatambua, Januari 29. Alikuwa muathirika ambaye alibadilishiwa kibao na kuonekana kama mtu aliyekuwa anaudanganya umma hali iliyosababisha watu kumhukumu mapema,” Wanasheria wake Tina Glandian na Patricia Browne Holmes wameeleza kwenye taarifa yao.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufutwa kwa mashtaka hayo dhidi yake, Jussie ameeleza kuwa hakuna sehemu ambayo aliudanganya umma na kwamba anawashukuru wale wote waliokuwa naye katika wakati huo mgumu.
Kwa upande mwingine, familia yake imetoa taarifa rasmi ambayo inaonesha kufurahishwa na uamuzi wa mahakama, huku wakiwakosoa vikali wale wote ambao walimhukumu kuwa ni muongo kabla suala husika halijathibitishwa.
Ama kweli jamii haipaswi kumhukumu mtu kwa kutumia tetesi au uchunguzi wa awali, hadi Mahakama itakapoamua kama ana hatia.