Serikali nchini, iliteua Timu ya Wataalam ambayo ilipewa jukumu la kufanya majadiliano na Wataalam wa Serikali ya Dubai na kufanikisha kuandaliwa na kusainiwa kwa Mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ujenzi, Prof. Makame Mbarawa Bungeni jijini Dodoma, na kuongeza kuwa mkataba huo ni kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari Tanzania.
Amesema, lengo la Mkataba huu ni kuweka msingi wa makubaliano (framework agreement) baina ya nchi na nchi ili kuwezesha kuanza kufanyika kwa majadiliano na kuingiwa kwa mikataba mbalimbali (Mikataba ya Nchi Mwenyeji, Upangishaji na Uendeshaji) ya uwekezaji na uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini.
“Mawanda ya uwekezaji chini ya Mkataba huu yatahusisha uendelezaji na uendeshaji wa baadhi ya maeneo ya Bandari na sio bandari yote kwa ujumla wake. Aidha, uendelezaji na uendeshaji huo utafanyika kupitia Mikataba Mahsusi ya Miradi (Project Agreements),” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, itajadiliwa na kuingiwa kwa kila eneo la ushirikiano na itahusisha matumizi ya ardhi pekee na sio umiliki wa ardhi ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakikisha kuwa Sheria, kanuni na taratibu za nchi zinazolinda umiliki ya ardhi ya Watanzania zinazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.