Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda kuwakamata madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini ili wajibu tuhuma za rushwa zinazowakabili.
Majaliwa aetoa agizo hilo leo Januari 4, 2021 baada ya kuzindua jengo la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga akiwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Madiwani hao wa kata za Mkumbi (Bruno Kapinga), kata ya Lukalasi (Bosco Ndimbo) na wa kata ya Linda (Haule) wanadaiwa kuchukua fedha kutoka kwa watendaji wa AMCOS kwa ajili ya kwenda kushawishi kuhamishwa kwa eneo la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa mvutano wa Madiwani wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini ambao baadhi yao hawataki makao makuu ya halmashauri hiyo yajengwe Kigonsera na kuamua kuendesha mchakato wa kushawishi wengine wagomee mradi huo jambo ambalo linakwamisha maendeleo kwa kuwa tayari mradi huo umeshaanza kujengwa.
Mvutano huo unaongozwa na Madiwani wa Kata tatu za Mkumbi, Lukalasi na Linda ambao wanataka makao makuu yajengwe kwenye kata ya Mkumbi katika eneo ambalo litailazimu Serikali ilipe fidia ya zaidi ya shilingi milioni 400 huku kukiwa na eneo la bure la ekari 150 ambalo ndiko yanakojengwa makao makuu.