Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi na kusema kwamba hajaridhishwa na baadhi ya majengo.
Amemwagiza Mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Tengamaso Wilson abomoe kuta zenye hitilafu na kurekebisha kasoro zilizopo kwenye majengo hayo ikiwemo kutonyooka kwa kuta.
Alitoa agizo hilo jana, wakati akikagua majengo ya hospitali hiyo, na kumweleza mhandisi kwamba kuta zimepishana unene kwa sababu hakusimamia kazi yake ipasavyo. “Ukuta huu ni mbovu kwa sababu hukuwasimamia vizuri mafundi wako. Kuna mahali juu unaona ukuta ni mdogo na huku chini ni mnene.”
Alipouliza ni kwa nini kumetokea tofauti baina ya kuta hizo, Waziri Mkuu alijibiwa kwamba tatizo ni upigaji wa lipu. na akatoa agizo “Mhandisi wa Wilaya simamia hili, kagonge upya kuta za jengo hili na lile. Hatuwezi kuwa na jengo la Serikali la aina hii. Tukitoa fedha ya Serikali ni lazima mjiridhishe kama kilichojengwa ndicho sahihi.”
“Tunahitaji majengo yote yawe ‘smart’, hata ujenzi wake nao uwe ‘smart’. Usikubali kutoa ‘certificate’ kama kazi haijakamilika. Kama kuna kazi haujaridhika nayo, usikubali ‘certificate’ itoke. Zile sentimeta 30 ni lazima zirekebishwe la sivyo, itaonekana huku uliweka matofali mengi kuliko upande ule,” alisisitiza.
Majengo ambayo Waziri Mkuu aliyakagua na kuonesha kutoridhishwa nayo ni ya utawala, wagonjwa wa nje (OPD) na maabara. Majengo mengine yanayojengwa ni jengo la wazazi, la X-ray, la utoaji dawa na la kufulia nguo.
Akiwa hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba katika awamu ya kwanza, Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la wazazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.
Ujenzi wa hospitali hiyo unafanyika kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalamu wa halmashauri na kamati mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza muweka hazina wa Halmashauri hiyo, Frank Chonya ajiridhishe na kazi za ujenzi zinazofanyika kabla hajaamua kutoa fedha za malipo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Andrea Chezue alisema kiasi chote kilichotolewa na Serikali cha sh. bilioni 1.5 kimeshatumika, na kwamba Halmashauri illitumia zaidi ya sh. milioni 100 ili kusafisha eneo na kulipa fidia ili wapate eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 56.