Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameahirisha vikao vya Mkutano wa Pili wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Machi 30, 2021.
Akizungumza wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu amesema kuwa serikali ipo kwenye utekelezaji wa kujenga shule mpya 1026, kwa kutumia mkopo wa Benki ya Dunia ili kusaidia elimu ya Tanzania na kupunguza uhaba wa shule na madarasa nchini.
“Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 30 Machi 2021 siku ya Jumanne saa 3:00 asubuhi katika ukumbi huu hapa jijini Dodoma”, amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza Simba SC kwa kupata ushindi wa kwanza ugenini kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita jana usiku Kinshasa, DR Congo.
“Nawapongeza pia mabingwa wa soka Tanzania timu ya Simba SC kwa kufanikiwa kufuzu hatua ya makundi na jana kushinda mchezo wake wa kwanza ugenini dhidi ya AS Vita nchini DR Congo,” amesema Majaliwa.
Simba ilishinda bao 1-0 dhidi ya AS Vita kwa mkwaju wa penalti uliowekwa wavuni na Chris Mugalu dakika ya 60 na kuipa uhakika wa alama tatu timu yake.