Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefarijika kuona Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), imeanza kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwadhibiti Tembo wanaovamia mashamba na makazi ya wanananchi, kwenye Wilaya za Nachingwea, Liwale na Ruangwa Mkoani Lindi.
Majaliwa, ameyasema hayo mara baada ya kupokea taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Dkt. Elbate Mjingo juu ya zoezi hilo uwanja wa ndege wa Nachingwea mkoani Lindi.
Amesema, Kamati za ulinzi na usalama kwenye Wilaya hizo zinatakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya utekelezaji wa zoezi hilo ikiwa pamoja na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ili kutosababisha wanyama kurudi kwenye maeneo ya makazi na mashamba.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu Dkt. Elbate amesema kuwa wamebaini uwepo wa makundi manne ambayo kati ya hayo matatu yapo Wilaya ya Nachingwea na moja lipo Wilaya ya Liwale na kusema “Kundi moja lina tembo 50, lingine tembo 20, lipo lenye tembo 5 na lipo la tembo 7, tumevalisha mkanda kwenye kundi moja la tembo na mengine tunatarajia kuyavalisha leo ili tuweze kufuatilia nyendo za kila kundi”
Rais Dkt. Samia, alipohutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba 1, 2022 uwanja wa Ilulu mjini Lindi aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuwatumia watalaamu wake kutekeleza agizo la kuwadhibiti tembo wanaovuka mipaka ya hifadhi na kuvamia makazi na mashamba ya wananchi.