Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Mauritius waje washirikiane na Watanzania katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya utalii, viwanda vya sukari, nguo na bidhaa za uvuvi.
Ameyasema hayo leo, (Jumatano, Agosti 28, 2019) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar katika Ukumbi wa Maonyesho wa Pasfico Yokohama nchini Japan.
Amesema kuwa nchi ya Mauritius ina uwezo mkubwa sana katika uzalishaji wa sukari na wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Watanzania katika kilimo cha miwa na ujenzi wa viwanda vya sukari na Tanzania ina ardhi nzuri na kubwa inayofaa kwa kilimo hicho pamoja na soko kubwa ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya sukari utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli za kuhakikisha inamaliza tatizo la upungufu wa sukari nchini.
Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, Waziri Mkuu amesema Mauritius imefanya vizuri sana katika utalii na hasa ule wa kutumia fukwe za bahari.
Kuhusu usafiri wa anga, Waziri Mkuu amesema kuwa wakati umefika sasa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza safari za kwenda Mauritius ili kuvutia watalii wengi wanaokwenda Mauritius kufanya utalii wa fukweni waje pia nchini.
“Watanzania wengi wameishia kuwekeza kwenye viwanda vya kuchambua pamba hivyo wanalazimika kuuza pamba yao nje ya nchi na wenzetu Mauritius wameenda mbali zaidi kwani wana viwanda vya nguo na viwanda vya nyuzi, kwa sasa Serikali ya Tanzania imeweka mkakati wa kujenda viwanda vya nguo ili kuongeza tija.”amesema Majaliwa
Amesema kuwa kwasasa wamekuabaliana na Waziri wa Mkuu huyo wa Mauritius kuwakutanisha Mawaziri wa viwanda na Biashara wa Mauritius na Tanzania wakae pamoja kwa ajili ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kuwashawishi wafanyabiashara wa Mauritius waje wawekeze katika viwanda vya nguo na nyuzi nchini.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo na Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya uwekezaji nchini ili kupata taarifa za kutosha zitakazomwezesha kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi yake waje wawekeze nchini.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.