Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kuanzia leo (Oktoba 20, 2022), kwa kampuni ya Inter Country Contractors kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa miradi ya barabara katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 20, 2022 alipokutana na Waziri wa Nchi -OR TAMISEMI, Viongozi wa Wilaya ya Ukerewe na Watendaji wa TARURA ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Amesema, kampuni hiyo ilipewa kandarasi ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 13 kwa kiwango cha lami na changarawe katika kisiwa hicho ambapo ilipaswa kukamilisha kazi hiyo Julai 2022.

Aidha, Majaliwa amesema ni vyema Mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mikoa na Wilaya wakatekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini na ukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angellah Kairuki amesema wamepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kuahidi kufanya mapitio makubwa ya mfumo wa kiutendaji wa TARURA ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ndani ya taasisi hiyo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 21, 2022   
Teknolojia ya Habari kuinufaisha nchi kiuchumi