Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mazishi ya mke wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakary Bin Zubeir yaliyofanyika Kwamndolwa, Korogwe mkoani Tanga.
Akitoa salam kwa niaba yake, Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Magufuli aliweka nia ya dhati kushiriki mazishi hayo lakini kwa bahati mbaya ana mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika jijini Arusha ambapo yeye ni Mwenyekiti.
“Mheshimiwa Rais amenituma nije nikupe pole wewe, watoto, familia na wote walioguswa na msiba huu. Mheshimiwa Rais anawaombea kwa Mungu ili mpate utulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na nguzo katika familia. haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.”amesema Majaliwa
Aidha, Majaliwa amewasihi wafiwa na waombolezaji wote waendelee kuwa watulivu na kumuombea marehemu kila mmoja kwa imani yake ili Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum akizungumza kwa niaba ya familia amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumtuma Waziri Mkuu amuwakilishe katika mazishi hayo. pia amewashukuru watu wote waliojitokeza kwa ajili ya kuifariji familia kutokana na msiba walioupata.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Salma Kikwete, Mhe. Hawa Ghasia, Mhe. Mary Chatanda ,Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigelana na Masheikh wa Mikoa.
-
JPM afanya uteuzi mwingine
-
Lugola awatangazia vita wauaji wa watoto, aeleza chanzo
-
Video: JPM apigilia msumari ma-DC kuwaweka watu ndani, Vyama vya siasa kubanwa fedha za ruzuku