Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuwa na mkakati wa maeneo ya uwekezaji kutokana na fursa ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ikiwemo kuchakata ujenzi wa kituo cha mabasi jirani na stesheni hiyo.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Novemba 24, 2022 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa stesheni kuu ya Dodoma eneo la Mkonze, jijini Dodoma, na kusema Serikali itahakikisha mradi huo haukwami na itakabiliana na viashiria vyote vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wake.
Amesema, Serikali inaendelea kufanya maboresho kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya usafirishaji na kuwataka Watanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huo kusimamia usalama wa mradi kuwa walinzi ili ukamilike kama ilivyokusudiwa na kutumia fursa mbalimbali zitakazowainua kiuchumi mara baada ya kukamilika kwake.
Awali, Mkurgenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema Shirika hilo lipo kwenye mpango wa ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ya mizigo na kwamba hadi sasa wamemesaini mkataba wa ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme 19, seti za treni 10 zenye uniti 80.
Amesema pia shirika hilo itanunua mabehewa ya kawaida ya abiria 89, mabehewa ya ghorofa 30 ambayo yanakuja, mabehewa ya mizigo 1,430 na vifaa vya matengenezo 26.
Hata hivyo, Serikali imesema imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa, na kusema itaendelea kuhakikisha mradi huo unajengwa kwa viwango na kukamilika kama ilivyopangwa na kuanishwa katika mkataba.