Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kuanzia Novemba 15, 2021 kwa wasimamizi wa Bonde la Mto Ruvu wafuatilie njia zote za kuingiza maji katika mto huo ambazo zimechepushwa ziwe wazi ili maji yaweze kuingia na kupunguza changamoto ya upungufu wa maji.
Amewaagiza wasimamizi wa mabonde yote nchini kutokukaa maofisini na badala yake wapite katika maeneo yote wanayoyasimamia na kuhakikisha yapo salama, huku akiwahasa Wizara ya Maji kutafuta chanzo kingine cha maji kitakachosaidiana na Mto Ruvu ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Aidha maagizo hayo ameyatoa leo Novemba 15, 2021 baada ya kutembelea vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo maalumu katika suala zima la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi hadi washio vijijini, Wizara ya Maji hakikisheni mnatafuta vyanzo vingine ili malengo hayo yatimie,” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema Mto Ruvu umeathirika na shughuli za kibinadamu zinazochangia maji kupungua, hivyo wahusika wasimamie ipasavyo ili kupunguza tatizo hilo. Amesema idadi kubwa ya mifugo katika maeneo hayo inaathiri chanzo hicho.
Sambamba na hayo yote Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza Wizara za Maji, Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi zikutane na kuona namna bora ya kuboresha mazingira ya ufugaji ili Mto Ruvu ubaki kwa ajili ya kuzalisha maji katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, lakini pia kuweka utaratibu wa kwa wafugaji ilin wasiharibu chanzo cha maji.
Naye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika mitambo ya kuzalishia maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kuhakikisha wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wanapata maji ya kutosha. “Vyanzo hivyo vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 520 huku mahitaji yakiwa ni lita milioni 544.”
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kwa sasa hali ya uzalishaji wa maji imepungua kutoka lita milioni 520 hadi lita milioni 460 kwa siku.
Amesema kupungua huko kunatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuwepo kwa makundi makubwa ya mifugo katika eneo la chanzo cha Mto Ruvu.