Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Wajumbe wa Halmashauri Kuu za Mkoa na Wilaya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wahakikishe wanakagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye maeneo yao na wajiridhishe kama inalingana na thamani halisi ya kiasi cha fedha kilichotumika.
Ameyasena hayo wakati akizungumza na viongozi wa CCM, wabunge pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Kigoma kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya CCM ya mkoa wa Kigoma.
Amesema kuwa iwapo viongozi hao hawataridhishwa na utekelezwaji wa mradi husika wasisite kuchukua hatua kwa kutoa taarifa katika ngazi husika, lengo ni kuhakikisha miradi yote inakuwa na ubora na inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
“CCM ni chama imara chenye mipango inayotekelezeka na kilicholenga kuwaletea wananchi maendeleo na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili na ndicho chama pekee chenye kuleta matumaini kwa Watanzania wote.”amesema Majaliwa
Aidha, Majaliwa amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi hao kujiridhisha na muenendo wa utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yao zikiwemo za afya, maji, elimu na kilimo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza wanachama na wapenzi wa CCM wasome katiba ya chama na kuzielewa kanuni, taratibu na sera ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. akisisitiza jambo hilo Waziri Mkuu amegawa nakala za katiba ya CCM kwa viongozi hao.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga amesoma taarifa ya mkoa huo, ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu linaloendelea kwenye mkoa huo.
-
Wachimbaji wa madini Njombe wampongeza JPM
-
Hukumu kesi ya Malkia wa Tembo imeiva
-
Hatufundishi askari wetu kuua watu- Kangi Lugola
Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2018 jumla ya wahamiaji haramu zaidi ya 4,135 walikamatwa kwenye msako uliofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.