Serikali imewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Cuba waje kuwekeza kwakuwa kuna fursa nyingi hapa Tanzania na kama zitatumika vizuri basi zitawezesha uchumi kuendelea kukua kwa kasi.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Havana nchini Cuba mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba, Lucas Domingo Polledo, ambapo amewakaribisha wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa.

Amesema kwa sasa Serikali ya Tanzania inaagiza dawa kutoka nje ya nchi jambo ambalo linasababisha kutumia fedha nyingi, hivyo uwepo wa kiwanda utasaidia katika kupunguza gharama.

Majaliwa ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini kama mkakati wa kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati, hivyo wafanyabiashara kutoka nchini Cuba wanakaribishwa kuja kuwekeza nchini, hususani katika viwanda vya dawa na sukari.

“Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.”amesema Majaliwa

Kwa upande wake, Balozi Polledo alisema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unaendelea kuimarishwa. Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

 

Video: Serikali yatangaza mfumo mpya wa usajili wa Magazeti
Breaking News: Kidao Wilfred Kaimu Katibu Mkuu TFF