Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezishukuru kada mbalimbali za Serikali, kiraia, Wasomi na vyombo vya Habari kwa kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambalo limefanikiwa kwa asilimia 99.9 na litasaidia katika upangaji wa shughuli za kimaendeleo.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Oktoba 31, 2022 katika zoezi la utangazaji wa matokeo ya Sensa ambayo yanatolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na kusema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zitawasaidia wafanyabiashara kutathmini uwezo wao wa kibiashara au uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji.
Amesema “Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuridhia kutekeleza sensa ya sita mwaka huu kinaonesha uimara wa uongozi wa Kiongozi wetu na utekelezaji wa takwa hili ni kwa faida ya nchi yetu na ulimwengu kwa jumla na zoezi hili ni muhimu na ni moja ya mikakati ya kiuchumi ya Taifa ya kuvutia uwekezaji na kuboresha kiwango cha maisha cha wananchi.”
Aidha, Majaliwa pia amevipongeza vyombo vya habari kwa ushiriki wao mkubwa katika kutoa hamasa kwa jamii na kuwaelezea umuhimu wa sensa na kwamba utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Julai, 2022 ulionesha kuwa asilimia 98 ya Watanzania wanatambua uwepo wa sensa.