Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi msaidizi na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili.
Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa leo Mei 28, 2021 inaeleza kuwa katika kikao kazi na Waziri wa Fedha na Mipango, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu wakuu na Watendaji waandamizi wa Wizara hiyo mkoani Dodoma jana, Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salum Hamdun kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikithibitika si za kweli wahusika warejeshwe kazini.
Majaliwa amezitaja tuhuma hizo kuwa ni malipo yaliyofanyika Machi 31, 2021 kupitia vocha 30 za Sh 251 milioni yakielezwa kuwa ni malipo maalum bila kutaja kazi maalum ni nini na nani aliifanya.