Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watafiti na wabunifu nchini kuongeza kasi ya kufanya tafiti ili nchi iende sambamba na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni kote.
Ametoa wito huo leo Mei 24, 2021 wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya sita ya wiki ya utafiti na ubunifu yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa ni lazima watafiti na wabunifu katika sekta zote wachukue hatua za makusudi katika kubuni na kutumia teknolojia zinazoibuka kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya viwanda na jamii yetu.
“Mabadiliko haya ya teknolojia yanatokea kwa kasi kubwa ulimwenguni yanachochewa na mwenendo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hivyo basi, nasi hatunabudi kujipanga vyema ili kuendana na kasi hiyo”.
Aidha, Waziri Mkuu amevitaka vyuo vikuu vyote nchini kuweka utaratibu wa kufanya utafiti na kisha kuonesha matokeo ya tafiti ili kusaidia kuimarisha uhusiano wa karibu baina ya vyuo na soko la ajira, Kadhalika ametoa wito kwa wenye viwanda kutoa ufadhili wa tafiti na bunifu zinazohusiana na bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vyao.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha tafiti ili taifa liweze kunufaika na teknolojia ya kisasa na kutoa huduma kwa jamii.