Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Idara wa Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo yao na wahakikishe inakamilika kwa wakati ili itae huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa mkoa wa Songwe akiwa kwenye majumuisho ya ziara ya kikazi mkoani Songwe ya kukagua miradi ya maendeleo na mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya sita imeyapata katika kipindi cha miaka miwili.
Amesema, “Huduma za jamii ndizo zinazogusa maisha ya kila siku ya wananachi kama elimu, maji, nishati, afya na kilimo, hivyo halmashauri zetu lazima ziongeze nguvu katika maeneo hayo. Wakuu wa Idara tumieni muda mwingi kwenda kwenye maeneo ambayo miradi inatekelezwa badala ya kukaa ofisini tu.”
Aidha Waziri Mkuu pia ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Mji Tunduma kwa kujenga baadhi ya miradi kwa kutumia makusanyo ya ndani ukiwemo ujenzi wa madarasa 10 katika shule ya msingi Haisoja kwa gharama ya shilingi milioni 800, amewataka viongozi wa halmashauri zingine nchini kuiga mfano huo.