Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itawachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhujumu ujenzi wa miradi ya maji mkoani Mara.
Waziri Majaliwa amesema hayo leo Januari 16, 2018 wakati alipokagua mradi wa maji wa Utegi uliopo katika kijiji cha Mika wilayani Rorya, ambapo ameeleza kuwa hiyo ni moja ya hatua zitakazochukuliwa kutokana na kutoridhishwa na utekelezwaji wa ujenzi miradi ya maji katika baadhi ya halmashauri za mkoa huo, hivyo kuwacheleweshea wananchi kupata huduma hiyo.
Amesema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Majaliwa amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
“Nitafuatilia katika maeneo yote ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maji kinalingana na thamani halisi ya miradi husika.”
Amesema anakerwa na Halmashauri ya wilaya ya Rorya kutosimamia vizuri miradi ya maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kutozingatia sheria.
Aidha, Majaliwa amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya wanaoshi wilayani Tarime wawe wamehamie Rorya ifikapo Februari 15, 2018.
“Atakayeng’ang’ania kuishi Tarime hadi siku hiyo atakuwa amejiondoa kazini mwenyewe. Lazima watumishi wote waishi kwenye vituo vyao vya kazi Rorya ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”
Pia amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo ulimaji wa bangi pamoja na uvuvi haramu na badala yake wafanye shughuli halali za kuwaingizia vipato.