Serikali imewataka wakazi walio katika Vijiji 14 vya eneo la Loliondo kuwa watulivu na hakuna atakaye waondoa katika makazi yao.
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 9, 2022, na kudai kuwa shughuli inayoendelea katika baadhi ya maeneo, ni kuweka alama (bicon) za maeneo yanayotakiwa kulindwa.
Amesema, alama hizo zinawekwa ili kulinda mapitio ya wanyama, mazalia ya wanyama na vyanzo vya maji na kwamba eneo la uwekaji huo wa alama lipo umbali wa kilometa nane kutoka moja ya kijiji cha Loliondo.
“Hakuna mtu atakayeondolewa katika eneo hilo na hakuna Askari ambaye alikwenda katika kijiji ndio maana ile video huoni askari yeyote,” amesema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, wapo baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema ambao wanataka kutengeneza taswira mbaya ndani na nje ya nchi, waliotengeneza video inayowaonesha wakazi wa eneo hilo wakiwa na mishale.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au mashirika yasiyo ya kiserikali (Ngos) yanaoeneza upotoshaji huo.