Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa walimu kuendelea kuimarisha huduma ya unasihi ili kuwawezesha wanafunzi hasa wa kike kupata stadi za maisha ambazo zitawapa maarifa na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni na maambukizi ya VVU.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaunga mkono tamko lililotolewa na Rais Samia aliyeweka wazi azma yake ya kuleta usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu kwa kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
”Serikali imeendelea kuimarisha mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi hususan wa kike ikiwemo kuongeza shule mpya za sekondari za wasichana za bweni kote nchini ili kutoa fursa kwa mtoto wa kike kukamilisha mzunguko wake wa masomo na hivyo kuweza kutimiza ndoto zake”. Amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa amesema Serikali imeshaweka mipango madhubutina mazingira mazuri ya mapokezi ya wasichana ambao walikatiza masomo kutokana na ujauzito.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kujenga shule 10 kati ya shule 26 zilizo katika mpango. Shule hizo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,200.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa zimesalia siku nane tu ili nchi ifikie kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru na kwamba namna bora ya kuadhimisha siku hiyo ni kwa Watanzania kujitathmini kila mmoja amelifanyia nini Taifa na kwa kiasi gani atashiriki katika kuliletea maendeleo.