Beki wa pembeni wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich David Alaba, ana mashaka ya kucheza mchezo wa ligi ya Bundesliga mwishoni mwa juma hili dhidi ya Hoffenheim, kufuatia majeraha ya kifundo cha mguu yanayomkabili.
Alaba amerejea klabuni hapo akitokea kwenye timu ya taifa lake, akiwa majeruhi baada ya kuumia wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Georgia siku ya jumanne.
Jopo la madaktari wa FC Bayern Munich limetoa taarifa kuhusu mchezaji huyo inayoeleza kuwa: “David Alaba anakabiliwa na majeraha ya kifundo cha mguu wake wa kushoto na huenda akashindwa kucheza mchezo wa mwishoni mwa juma hili, aliumia katika mchezo dhidi ya Georgia dakika ya 38.
“Ana uwezekano mdogo wa kucheza mchezo dhidi ya Hoffenheim, kutokana na hatua za kupatiwa matibabu kuendelea klabuni hapa kwa sasa, kama itashindikana kupita katika vipimo vya mwisho, atalazimika kukaa nje hadi hapo hali yake itakapotengemaa.”
Wakati huo huo jopo hilo la madaktari limetoa taarifa njema kwa mashabiki wa The Bavarians kuhusu maendeleo ya Sebastian Rudy, ambaye aliumia wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia kati ya Ujerumani dhidi ya Norway waliokubali kisago cha mabao 6 kwa 0.
Rudy aliyesajiliwa na Bayern Munich akitokea 1899 Hoffenheim mwezi July mwaka huu, hakumaliza mchezo huo kutokana na majeraha ya mguu na leo alitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kwa ajili ya mazoezi ya kuelekea mchezo wa jumamosi.