Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger, amekanusha taarifa za kuzuka kwa hali ya kutoelewana kati yake na mshambuliaji Alexis Sanchez, baada ya dili la uhamisho wake kukwama siku ya mwisho kabla ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi halijafungwa nchini England.

Wenger amekanusha taarifa hizo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mapema hii leo kaskazini mwa jijini London, ambao ulihusu maandalizi ya kikosi chake kuekekea mchezo wa ligi wa mwishoni mwa juma hili, ambapo The Gunners watakua wenyeji wa AFC Bournemouth.

Babu huyo kutoka nchini Ufaransa amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote, na kinachoendelea katika vyombo vya habari ni sehemu ya uchokonozi ambao unadhaniwa huenda ukamkosanisha na mshambuliaji huyo kutoka Chile.

“Hakuna jambo kama hilo, hapa hali ni shwari kama ilivyokua siku za nyuma, nimekua nazungumza na Sanchez tangu alipoondoka hapa London kwenda kwenye timu ya taifa lake, na hajawahi kuniambia lolote kuhusu kukasirishwa na uamuzi wa kugoma kumuuza wakati wa majira ya kiangazi.”

Kuhusu maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya AFC Bournemouth, Wenger amesema mambo yanakwenda vizuri, na anatarajia mchezo huo utakua na kila sababu ya kikosi chake kurekebisha makosa waliyoyafanya kwenye michezo miwili iliyopita.

“Tunaendelwa vizuri na hatua za kujiandaa kuwakabili AFC Bournemouth jumamosi, naamini makosa tuliyoyafanya katika mchezo dhidi ya Stoke City na Liverpool hayatojirudia tena.”

Wakati huo huo Wenger ametoa taarifa kuhusu maendeleo ya kiungo Santi Cazorla aliye majeruhi kwa sasa, kwa kusema huenda akarejea uwanjani kabla ya Krismasi.

Majareha yamuweka shakani David Alaba
Waziri Simbachawene ajiuzulu