Serikali Nchini, imesema Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR, unaendelea vizuri na kwasasa inakamilisha baadhi ya taratibu za Mazingira na Jamii kwa mujibu wa viwango vya Kimataifa na kufanyia kazi taratibu za upatikanaji wa rasilimali fedha kwa kipande cha tatu na nne cha ujenzi na majaribio ya usafiri huo yatafanyika Desemba 2023.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba jijini Stockholm nchini Sweden, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Dhamana la nchi hiyo – EKN, Anna-Karin Jatko, ambalo limetoa dhamana kwa mabenki mbalimbali yanayotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa SGR.
Amesema, nchi hiyo pia ilitoka dhamana kwa ajili ya upatikanaji fedha kwa kipande cha kwanza na pili ya SGR kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Makutupora – Singida, ambao ujenzi wake umefikia asilimia 98 wa loti ya kwanza na asilimia 95 wa loti ya 2 na inatarajiwa kuanza majaribio hayo ya uendeshaji Desemba.
“Reli hii yenye urefu wa kilometa 2,102 ni muhimu kwa maendeleo na uchumi wa nchi na ni mradi wa kimkakati wa kikanda na ni kipaumbele cha nchi kwa hivi sasa kwa sababu utakuwa na matokeo makubwa kijamii na kiuchumi utakapo kamilika,” amesema Dkt. Mwigulu.