Taarifa zinaeleza kuwa Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi amepewa adhabu ya kukaa nje ya Uwanja kwa Majuma mawili na Uongozi wa Klabu ya Paris Saint-Germain, baada kuonekana akiwa Saudi Arabia na familia yake bila ya ruhusa.
Messi aliondoka jijini Paris hadi Saudi Arabia kutokana na ishu za kibiashara akiwa kama balozi wa nchi hiyo, lakini Uongozi wa PSG ulichukizwa na kitendo cha staa huyo kukwepa mazoezi.
Ikumbukwe Messi alikubali kusaini kitita cha Pauni 25 milioni aitangaze Saudia Arabia kwa kuitembelea nchi hiyo kwa wiki mara moja.
Lakini kwa mujibu wa ripoti Messi aliondoka jijini Paris bila kupewa ruhusa na uongozi wa PSG inayonolewa na Christophe Galtier, pia hakumjulisha mkurugenzi wa michezo, Luis Campos.
Sasa kufuatia hatua hiyo ya Messi miamba ya hiyo ya Ufaransa imempa adhabu na hataungana na wachezaji wenzake kwa muda wa wiki mbili, huku taarifa zikiripoti kwamba PSG haitamuongezea mkataba mpya.
Hiyo inamaanisha kwamba Messi atakosa michezo miwili ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) dhidi ya Troyes mwishoni mwa juma hili, kisha dhidi ya Ajaccio ambao utachezwa Mei 13.
Gazeti la The Sun lilijaribu kuwatafuta wawakilishi wake wathibitishe taarifa hiyo, lakini hawakupatikana.
Messi, 35, alitupia picha yake kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa nchini Saudi Arabia pamoja na familia yake wakifurahia mandhari za nchi hiyo.
PSG ilipokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Lorient mwishoni mwa juma lililopita kabla ya Messi hajakwea pipa kwenda Saudi Arabia.
Kufuatia kipigo hicho miamba hiyo sasa ipo kileleni kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Marseille ambayo ina alama 70 ikiifukuzia kwa karibu katika mbio za ubingwa.