Majina ya watu wanaotuhumiwa kukisaliti Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, yamechukua nafasi ya aina yake katika vikao vya kamati za chama hicho zilizokutana mjini Dodoma kabla ya Mkutano Mkuu.
Taarifa kutoka Mjini humo zimeeleza kuwa juzi Kamati ya Maadili ilishindwa kumaliza ajenda ya kikao chake iliyojumuisha majina ya wasaliti, hali iliyosababisha kikao cha Kamati Kuu (CC) pia kusogezwa mbele kwani kamati hiyo hukaa kujadili pamoja na mambo mengine ajenda na yatokanayo na kikao cha kamati ya maadili.
“Tulitegemea siku moja au mbili zingeweza kutosha kwa Kamati ya Maadili kumaliza suala hilo [la majina ya wasaliti] lakini inaonekana kama jambo hilo limekuwa gumu na kamati inakutana kwa siku ya tatu mfululizo (jana),” mmoja wa chanzo kilieleza kwa sharti la kutotajwa jina.
Chanzo kingine kilieleza kuwa huenda kikao cha Kamati ya Maadili kiliamua kuyapitia majina ya watuhumiwa wa usaliti katika ngazi zote, majina ambayo yalitokana na kamati ndogo iliyoundwa kufanya kazi ya kuyabaini majina hayo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania bara), Phillip Mangula.
Baada ya vikao vya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu ya chama hicho tawala, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu vinatarajiwa kufanyika kuanzia leo mjini Dodoma, lengo kuu likiwa kufanya mabadiliko makubwa.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, Rais Magufuli aliahidi kuwashughulikia wanachama wote ambao walikisaliti chama hicho na kuusaidia upande wa upinzani huku wakiwa bado ndani ya chama hicho.