Wachezaji wa Klabu ya Yanga wamepania kutikisa nyavu za wapinzani wao Zanaco kutoka Zambia, ingawa wako katika hali mbaya kifedha wakidaiwa kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu.

Yanga inatarajiwa kuivaa Zanaco leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kufuzu katika hatua ya pili ya kombe la Klabu Bingwa barani Afrika.

Mechi hii ni muhimu kwa mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Tanzania bara kwani endapo watashinda watafuzu katika hatua ya makundi lakini mambo yakienda kombo watalazimika kushushwa kucheza katika mechi za mtoano za Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Wachezaji hao wanadaiwa kupeana moyo katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana, wakiamini kuwa endapo watafanya vizuri viongozi watahamasika na kuwalipa mishahara yao ya miezi mitatu inayodaiwa kukwama.

“Ninaamini kuwa, kama tukishinda mechi hii viongozi watahamasika na kushawishika kutulipa mishahara yetu ya miezi mitatu, hivyo kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza, basi anatakiwa kupambana ili tushinde mchezo huu,” mmoja wa wachezaji amekaririwa na blog ya Saleh Jembe.

Yanga ambayo hivi karibuni ilijeruhiwa kwa kupoteza mchezo dhidi ya watani wao wa jadi, Klabu ya Simba baada ya kushindwa 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayodhaminiwa na kampui ya simu ya Vodacom, wako katika wakati mgumu huku Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji akiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano, huku akiwa na kesi mahakamani kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.

Matapeli wajinufaisha kupitia jina mama Salma Kikwete
‘Majina ya Wasaliti’ yavipa wakati mgumu vikao Kamati za CCM Dodoma