Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu uwepo wa Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos), inayotapeli watu fedha kwa kutumia majina ya watu maarufu nchini.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini humo.
Amesema Saccos hiyo yenye jina maarufu la Focus Vicoba kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na tovuti inayojulikana kwa jina “http://www.vicobaloanstz. wapka-mob” www.vicobaloanstz. wapka-mob, hutumia majina ya viongozi wa Serikali na watu maarufu, kwa nia ya kuwatapeli wananchi.
Aidha, majina ya viongozi na watu maarufu yanayotumiwa na matapeli hao ni pamoja na jina la Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
“Nitoe onyo kwa wale wote wanaoendelea kufanya udanganyifu huu wa kujipatia fedha kwa njia isiyo halali kupitia mitandao ya kijamii kuacha mara moja, kwani sheria iko wazi na pindi watakapokamatwa, watachukuliwa hatua kali,”amesema Sirro.
Vile vile, Sirro amesema kuwa katika ufuatiliaji wa suala hilo, kitengo cha upelelezi wa makosa ya mitandao cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kimebaini kuwa katika tovuti “http://www.vicobaloanstz. wapka-mob” www.vicobaloanstz. wapka-mob picha na jina la Mama Salma, limetumika huku kwenye ukurasa wa Facebook wakitumia jina la Mengi, likiwa ni pamoja na namba za simu ambazo ni 0757 308381 na 0768 199359 ambazo si za Mama Salma wala Mengi.
Hata hivyo, Kamanda Sirro amewaasa wananchi wote, kutokuwa wepesi kukubali matangazo ya mikopo, yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii, bila kufika katika ofisi husika ili kujiridhisha kuhusu utolewaji wa mikopo hiyo, ili kuepuka kutapeliwa fedha na mali zao.

Sophia Simba atimuliwa CCM kwa usaliti, Nchimbi na wenzake walimwa...
Yanga yaipania Zanaco licha ya kuwa ‘vibaya’ mifukoni