Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo na Al Hilal Omdurman ya nchini Sudan Glody Makabi Lilepo rasmi ameomba kuondoka katika klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Khartoum.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu mshambuliaji huyo kuwepo katika rada za kuwaniwa na klabu kongwe za Tanzania Simba SC na Young Africans kuelekea usajili wa dirisha kubwa.
Young Africans hivi sasa katika mipango ya kukisuka kikosi hicho ili kifanye vema katika msimu ujao ambao timu hiyo, inakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mmoja wa mabosi wa Young Africans amesema, kuwa sababu kubwa ya mshambuliaji huyo kuandika barua ya kuomba kuondoka ni kulinda kipaji chake.
Bosi huyo amesema kuwa mshambuliaji huyo ameomba kuondoka kutokana na nchi hiyo, kukabiliwa na vita ambayo inaendelea huko Sudan.
Ameongeza kuwa Young Africans itamsajili mshambulaiji huyo kama mchezaji huru mara baada ya yeye mwenyewe kukubali kuvunja mkataba huo Al Hilal ambaye aliisaidia kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
“Lilepo ameomba kuondoka ili alinde kipaji chake baada ya Sudan kukabiliwa na vita na tayari Young Africans, yupo tayari kumsajili mshambuliaji huyo katika kuiboresha safu hiyo.
“Tunafahamu baadhi ya klabu ikiwemo Azam FC na Simba zimeingia vitani kuitaka saini yake, lakini ninaamini sisi tutampata,” amesema bosi huyo.
Lilepo amezungumzia hilo kwa kusema: “Nipo katika mazungumzo mazuri na Young Africans, kama yakienda vizuri basi nitasaini huko.”