Tanzania ni moja ya nchi katika Bara la Afrika inayokabiliwa na kuendelea kushamili kwa matukio ya kinyama ya mauaji ya watu wenye ualbino kutokana na baadhi ya waganga wakienyeji wanaotumia ramli kutokuwa na elimu ya matumizi ya nyota.
Ramli ni chimbuchimbu ya kubaini matatizo kwa kutumia nyota pasipo kutumia sayansi elimu ambayo hutumiwa na watu waliopata elimu hiyo.
Elimu ya nyota hutolewa zaidi katika nchi ya kiarabu kupitia mafunzo maalumu ya sayatulkhabar.
Matumizi mabaya kwa kukosekana kwa elimu hiyo kumesababisha kushamiri kwa matukio ya kinyama ya mauaji ya watu wenye ualbino na mengineyo.
Tangu nchi yetu ipate uhuru wake mwaka 1961 serikali kupitia idara ya ustawi wa jamii imekuwa ikitoa huduma kwa watu wenye ulemavu bila kuwa na sera timilifu.
Kuwepo kwa sera ya taifa ya maendeleo na huduma na watu wenye ulemavu matokeo ya miaka mingi ya majadiliano baina ya serikali na wadau wanao jishughulisha na mambo yanayowahusu walemavu.
Kimataifa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu hususani mikataba ya haki kwa watu wenye ulemavu [1975], haki za mtoto [1989], na haki na fursa sawa kwa watu wenye ulemavu [1993] hii ni kwa lengo la kulinda na kutetea haki zao.
Kutokana na hilo Tanzania imekuwa ikishirikiana na mataifa mengine dunia kuhakikisha ukamilishaji wa mikataba kuhusu ulinzi na uboreshaji wa haki na hekima kwa watu wenye ulemavu.
Tanzania ni nchi pekee inayowastaajabisha watu wa mataifa mengine duniani kutokana na kuweka historia ya mauaji ya watu wenye ualbino kwa madai mbalimbali ikiwemo imani potofu za kishirikina ambapo wauaji wanaamini kuwa sehemu za viungo vya watu hao zinaweza kuleta utajiri katika maisha yao.
Wasababishi wakuu wa mauaji hayo ni waganga wa kienyeji ambao huwashawishi wateja wao kwa dhumuni la kupata utajiri au kufanikiwa katika maisha.
Mauaji ya watu wenye ualbino ni dhahiri kuwa yanaleta simanzi kubwa katika jamii huku ikushuhudiwa mauaji ya kuhuzunisha ya watu wenye ualbino na wakati mwingine hupelekea hata kupoteza viungo vyao vya mwili pamoja na vifo kwa kuchinjwa kama wanyama pasipo wahusika kuchukuliwa hatua kali ambazo zitawafanya wauaji hao kuogopa kuendelea kufanya mauaji hayo.
Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 14 inasema kila mtu ana haki yakuishi na kupata hifadhi ya maisha yake katika jamii.
Kupitia vifungu hivyo vya sheria inawezekana kabisa wauaji hawavitilii maanani vifungu hivi vinavyotaka haki ya kuishi ya kila raia iheshimiwe. Hivyo basi kuendelea mauaji ya albino ni ukikwaji wa haki za binadamu unao paswa kulaaniwa pamoja na wahusika kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine walio na nia kama hiyo.
Akizungumza katika makala hii mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Nabroho lenye makao yake makuu mkoani Simiyu, Nkondo Kubini amesema kwa sasa wanatekeleza mradi wa uwajibikaji katika kulinda na kutetea haki za watu wenye ualbino anasema kuvamiwa kwa tasinia na taaluma hiyo kumesababisha kushamiri kwa ukatiri na kuvunjwa kwa haki za watu wenye ualbino .
Anasema hapa Tanzania waganga wengi wa kienyeji hutumia mizimu, majini na tunguli kutambua matatizo ya wateja wao kitu ambacho baadhi yao hutumia mwanya huo kuwadanganya wateja na kusababisha mauaji kwa baadhi ya watu hasa wenye ualbino.
Anasema baadhi ya waganga wa ramuli wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwadanganya wateja wao kutafuta viungo vya watu wenye ualbino ili watengeneze dawa kwa lengo la kujipatia kipato kitu ambacho kimechangia kuwepo kwa mauaji ya watu hawa.
Ameongeza kuwa kutokana na kushamiri kwa matukio hayo serikali imetangaza kuwepo kwa kikosi kazi cha kupambana na waganga matapeli na wauaji wa watu wenye ualbino.
Kubini anasema ili Serikali ifanikishe zoezi hilo iwashirikishe wataalamu wa tiba mbadala kuwasaka waganga wanaotumia ramri ili kutokomeza vitendo vya kikatili nchini.
Amesema ni ukweli ulio wazi kuwa pamoja na serikali kupiga marufuku shughuli za waganga wa ramri chonganishi ni wazi haitaweza kubaini watu hao pasipo kushirikiana na matabibu kwani waganga wetu wanao tumia ramri chonganishi wamekuwa wakiendesha shughuli zao maeneo ya vichochoroni huku wengine wakifanya kazi hii majumbani kwao.
“Ili kufanikisha zoezi hili ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kutushirikisha ili kuwabaini watu hao na kurejesha imani kwa watu wenye ualbino kama ilivyokuwa miaka ya nyuma”. anasema kubini.
Maganga Ndaki ni katibu wa waganga wa jadi anasema kuwa serikali ifanye zoezi hili kuwa endelevu kwani udhaifu unaofanywa na watendaji katika mazoezi mengi umesababisha vitendo viovu vingi kukoma kwa muda.
Pia anaitaka serikali kuunda kamati za kudumu itakayosimamia shughuli hizi nchi nzima nakuitaka kamati hiyo kuhakikisha inafanya kazi kwa nguvu ili kukomesha mauaji ya watu wenye ualbino.
Anawashauri waganga wa kienyeji wasio na elimu ya nyota kusoma elimu hiyo kabla ya kupiga ramri kwani kufanya hivyo mbali na kuchochea mauaji ya albino pia vinachangia kuongeza umasikini wa watu.
Miaka ya nyuma kulitokea kwa kushamiri kwa matukio ya kinyama ya mauaji ya watu wenye ualbino serikali ya mkoa wa Simiyu ilitangaza mikakati maalum ya kupambana na mauaji hayo na kufanikiwa kwa asilimia 99 mpaka sasa.
Mikakati hiyo itahakikisha vitendo hivyo vya kinyama na ukatili vinatokomezwa nchini zoezi ambalo litaanzia mikoa vinara wa matukio hayo ukiwepo mkoa wa Simiyu, Mwanza, Singida, Geita, Tabora na Shinyanga.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthon Mtaka amesema mikakati mbalimbali imefanikiwa kutokomeza kabisa mauaji ya watu wenye ualbino katika mkoa wa Simiyu kwani yapata miaka 3 sasa hakuna tukio la kuuawa kwa mtu mwenye ualbino na hata vikongwe.
Pia chama cha watu wenye ualbino (TAS) kimehusishwa katika oparesheni hiyo ambayo itaanza katika mikoa hiyo.
Hii oparesheni tokomeza mauaji ya albino tutasimamia kikamilifu ili kuhakikisha kila mtanzania anapata haki ya kuishi. “Serikali haiwezi kuvumilia matukio ya kinyama” amesema.
Mtaka ameongeza kwa kusisitiza kuwa kazi hiyo itaanzia katika mikoa inayoonekana kushamiri kwa vitendo hivyo na kisha kusambaa nchi nzima.
Naye Mwenyekiti wa TAS, Ernest kimaya amesema kamati hiyo itaongeza kuwepo kwa nguvu ya pamoja ya kukomesha vitendo viovu.
Amesisitiza kwa kuitaka kamati hiyo kuwakamata watu hao bila kuwaonea haya wote wanaojihusisha na ukatili huo na kuwafungulia mashitaka kwa wakati.