Grace Mugabe alitajwa kuwa ni moja ya chanzo cha anguko la Mugabe kisiasa ikihusu mamlaka na mahaba na huenda si wengi wenye kujua mahusiano ya kimapenzi ya Robert na Sally ya miaka hiyo ya nyuma yaliyopelekea ndoa na hata wakapata mtoto mmoja aliyekuja kufa kwa malaria akiwa na miaka mitatu tu.
Naam, ametokea wapi huyu Robert Mugabe, mwana wa pili kati ya wana watatu wa baba yake, Fundiselemala wa kijijini, Mzee Mugabe? tumeona kuwa Robert aliyezaliwa mwaka 1924 utotoni alikuwa mtulivu sana. Ndoto yake ilikuwa ama aje kuwa Mchungaji au Mwalimu wa shule.
Robert alishuhudia kaka yake Michael kwenye umri wa miaka 15, akifa kwa kula sumu ya majani wakiwa pamoja porini. Robert akabaki na mdogo wake tu na Baba yake akaja kuitelekeza familia yao. Robert na mdogo wake wakalelewa na mama yao.
Hatimaye Robert akaja kuwa mwalimu kwenye shule ya msingi ya kijijini kwao, Kutama, Chinoyi. Robert tangu utotoni akawa ni mwenye bidii ya masomo. Robert aliifariki dunia akiwa ni mwenye digrii saba. Tatu kati ya hizo alizipata akiwa gerezani, mojawapo ni ya sheria.
Sally kwenye maisha ya Mugabe
Robert alikutana na Sally alipokuwa akisoma Ghana. Walipendana na wakaoana mwaka 1961. Sally ni raia wa Ghana na waliamua kuishi wote Salisbury ( Sasa Harare). Robert akaingia matatani kisiasa na kufungwa mwaka 1964. Ni kwa miaka kumi.
Mwaka mmoja kabla ya kifungo, walimzaa mwana wao pekee, Nhamodzenyika, ikiwa na maana ya nchi inayoteseka. Kwa kifupi walimwita Nhamo.
Sally ambaye alikuwa mcheshi na msomi, alichangia sana kumjenga Robert hata kumsaidia kupata marafiki wa kuongea, maana, Robert ujanani alikuwa ni mkimya sana na asiyependa kujichanganya na watu.
Mugabe akiwa gerezani Zimbabwe, Sally alilazimika kukimbia Zimbabwe na kwenda kuishi kwao Ghana. Mwana wao Nhamo alifariki kwa malaria akiwa na miaka mitatu tu. Robert aliomba ruhusa ya bwana gereza ili akamzike mwanawe Ghana alikoishi Sally. Alikataliwa. Jambo hilo lilimhuzunisha sana Robert.
Mwaka 1974 Sally aliungana tena na Robert aliyetoka gerezani. Walikutana kwenye uwanja wa mapambano ya ukombozi. Ni kule Msumbiji.
Sally baada ya Uhuru wa Zimbabwe 1980, aliishi na mumewe Ikulu ya Harare. Sally alipendwa sana na Wazimbabwe. Wakazoea kumwita ‘ Amai ‘ ikiwa na maana ya ‘ Mama Yetu’. Hata hii leo, Sally Mugabe anaonwa kama ‘ Mama wa Taifa’ la Zimbabwe.
Grace kwenye maisha ya Mugabe.
Grace Marufu ni msichana mrembo aliyezaliwa Afrika Kusini. Alifanya kazi ya Ukatibu Mukhtasi kwenye Ikulu ya Robert Mugabe. Ndipo hapo mahusiano ya kimapenzi kati ya Robert na Grace yakaanza huku Robert akiwa kwenye ndoa na Sally, lakini, wakiwa wapweke bila hata mtoto baada ya mwana wao Nhamo kufariki.
Grace akapata ujauzito wa Robert. Ni mwaka 1988. Haikufanywa siri, Sally akajulishwa na akakubali hali hiyo mpya na mwaka 1992 Sally Mugabe alifariki kwa kuugua homa ya mapafu. Mwaka 1996 Robert na Grace wakafunga ndoa. Grace Marufu akawa Grace Mugabe, First Lady.
Kuna ya kutafakari juu ya uongozi na mahusiano ya kimahaba. Wengi wanafikiri, kama angelikuwepo, kuwa Sally Mugabe angeliweza kumsaidia zaidi Robert Mugabe kiuongozi na pengine Robert Mugabe asingefikia hatua ya kung’ang’ania madaraka.
Kuna wenye kuiunga mkono nadharia hii. Maana, ni kama Sally alimjenga Robert na Grace akaja kumbomoa Robert. Na hakika, Robert wa Sally hakuwa na makuu.
Robert alikuwa mtu ‘ Simpo’ sana. Hakuwa wa matumizi ya anasa. Yumkini Grace aliyekuwa nusu ya umri wa Robert hakutokea kwenye mazingira ya Robert na wala hakujikita kwenye falsafa ya Robert. Kimsingi, kama Sally, Robert alikuwa Mjamaa.
Kuna mengi ya kusimulia juu ya mahusiano ya Sally na Robert na namna Sally alivyomsaidia kumjenga Robert kisiasa katika ujana wao. na yapo ya kusimulia pia, namna Grace alivyochangia kwenye anguko la Robert kisiasa.
@ Maggid Mjengwa.