Na: Josefly Muhozi
Enzi za Mwalimu… hatukuhitaji ‘upepo wa kisulisuli’ kutuletea mke au mume kama ulivyowaletea wana wa Israeli ‘nzige’ wakiwa jangwani, ‘walipozimiss’ nyama walizokula utumwani Misri!
Haikuwa rahisi kuoa au kuolewa lakini uhitaji wake ulikuwa wa hali ya juu kiasi kwamba ni sawa na kusema ilikuwa ‘lazima uoe au uolewe’. Kwa mwanaume ilikuwa ni lazima uoe, au ukubali kuitwa ‘hohehahe wa maisha’ usiye na maana kwani hautakuwa na ‘mji’ hata kama una nyumba nzuri kiasi gani. Kwa maana ya kabila moja la Kanda ya Ziwa usiyeoa wakati muda umefika ungeitwa ‘Omtabhakanu’. Waliamini ‘apataye mke amepata kitu chema’.
Kadhalika, ili umpate mwenza, baada ya kumtaja msichana unayekusudia kumuoa, au hata kama umeoneshwa na wazazi wako ilibidi iundwe kamati ya wazee na vijana itakayofanya uchunguzi wa kina na usaili wa siri ili kujiridhisha kama unayetaka kumuoa ‘anafaa au la’!
Kamati ilifukunyua kila kona, hadi ndani ya ukoo wa binti anayechumbiwa ili kufahamu kama yaliyomo yamo? Kwani waliamini ‘maji hufuata mkondo’. Kwa ufupi ilikuwa zaidi ya ‘vetting’ wanayofanyiwa watu wanaotaka kupewa nafasi nyeti kwenye ofisi za Serikali. Waliamini pamoja na ulazima wa kuoa, ‘ni bora ukosee njia kuliko kukosea kuoa’. Na ndoa zilidumu hata watu walisahau kama kuna kusherehekea ‘anniversaries’ kwani kudumu ilikuwa suala la kawaida tu bali kuachana ilikuwa aibu.
Lakini sasa, mambo yamebadilika. Mchungaji, Dkt. Getrude Lwakatare ambaye wiki iliyopita alianzisha maombi ya ‘upepo wa kisulisuli’ kuwaombea wanawake akisisitiza kuwa ndoa ndiyo taasisi ya kwanza aliyoianzisha Mwenyezi Mungu duniani, anasema, “wanaume wamekuwa bidhaa adimu sana.”
Februari 14, 2017, Siku ya Wapendanao, mrembo wa Australia, Linda Liv Doktar aliamua kujioa mwenyewe baada ya kuachana na mpenzi wake, aliona hana matumaini tena ya kumpata mwanamme wa kumuoa. Ipo mifano lukuki ya wanawake kufunga ndoa na wanyama kama paka, mbwa… basi tu ili mradi wakamilishe ndoto yao ya kuolewa. Dunia ina mambo wewe..!
Sasa usichanganywe na idadi ya honi za maharusi kila wikendi mijini, hao ni wachache waliobarikiwa kama sio kubahatisha… na kwa bahati mbaya baadhi wanaposhindwana na kuachana hawapiti tena barabarani na matarumbeta ili tuwaondoe kwenye kumbukumbu zetu!
Baadhi ya wanaume nao wanalalama kuwa wanawake wamechotwa na maisha ya mitandaoni na wamekuwa bidhaa unayopaswa kuinunua kwa tahadhari kubwa sana.
Kuna mzee mmoja aliniambia, uzinzi umepunguza utamu wa ndoa, wengi wanafaidi matunda ya ndoa bila ndoa kwahiyo wanaona kwanini ufuge ngómbe kama unauweza kupata maziwa kirahisi tu! Lakini hawa wanywa maziwa bila kufuga ngómbe wasisahau adhabu ya bakora mia moja hadharani iliyotajwa kwenye Quran Takatifu dhidi yao isipokuwa wakitubu na kumrudia Mwenyezi Mungu. Na Kitabu Kitakatifu kimeeleza kuwa wazinifu wataoa wanawake wazinifu na washirikina, vivyo hivyo kwa wanawake wazinifu. Na yote ni haramu.
Lakini Je, watafiti wa dunia ya sasa wamebaini nini baada ya kuwahoji vijana wa kike na wakiume pamoja na waliopitwa na umri wanaotegemewa kuwa kwenye ndoa?
Utafiti uliofanywa na gazeti la PM Express la nchini Nigeria umebaini kuwepo idadi kubwa ya wanawake wanaolalamika kukosa wanaume wenye sifa za kuanzisha nao familia, kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, wanawake wengi wameeleza kuwa wamekosa wanaume wa kuolewa nao kwa sababu ya kukosa matumaini ya siku za usoni za wanaume wanaowachumbia kuwa na sifa za kuwa baba bora wa familia. Sababu nyingine ni kukosa wanaume walio na utayari kuoa.
Ripoti imebaini kuwa wanawake wengi wanaona bora kuishi peke yao au kuishi nyumbani kwao kuliko kuishi na mwanaume ambaye maisha yake ya usoni hayaoneshi mwanga wa kumudu maisha.
Lakini pia, wanaume wenye umri mkubwa waliohojiwa ambao hawajaoa, wengi wao walieleza kuwa ni bora waishi peke yao kuliko kuingia katika maisha ya ndoa ili hali hawana uhakika wa vipato vya kumudu maisha ya kisasa ya wanawake wa kisasa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wengi wenye umri mkubwa wameonesha kulalamika kukosa wanaume ingawa wanatamani kuolewa, huku wakidai kuwa muda wao kiafya wa kuzaa watoto (ukomo kati ya miaka 45-50) unawapa wakati mgumu.
Karia Anumba, mwenye umri wa miaka 41, mmoja kati ya wanawake waliohojiwa na PM.PRESS ameeleza kuwa amezunguka majiji kadhaa nchini humo akijaribu kumpata mwenzi wake bila mafanikio. Ameeleza kuwa wachumba wengi aliofanikiwa kuwa nao katika baadhi ya majiji walionesha kuogopa kuoa kwa madai ya kutokuwa na uhakika wa maisha ya ndoa.
Ameeleza kuwa akiwa Abuja, aliwapata wanaume kadhaa aliokuwa na uhusiano nao, lakini licha ya kuwashawishi kuwa angeweza kuhudumia familia yeye mwenyewe kutokana na kipato chake, hakuna aliyekubaliana naye kufikia hatua ya kufunga ndoa.
Anumba ameeeleza kuwa alihamia Lagos kikazi akitokea Abuja, lakini kutokana na msako wake wa mwanaume wa maisha yake alifikia hatua akajiona kuwa anageuka kuwa kahaba kutokana na ongezeko la idadi ya wachumba.
Gazeti hilo limemkariri pia Doris, ambaye ana umri wa miaka 39 (jina la baba yake limehifadhiwa), ambaye alidai kuwa amewahi kuwa na wachumba wengi na kuwaonesha maisha ya mapenzi yaliyo na raha lakini hakuna hata mmoja aliyekubali kufikia hatua ya kufunga naye pingu za maisha. Amesema wengi walidai kuwa hawako tayari kiuchumi kutokana na ukosefu wa ajira pamoja na misukosuko ya kiuchumi nchini humo.
Tony Nweje, mwanaume mwenye umri wa miaka 44 ambaye hajaoa alipoulizwa, alieleza pia kuwa anatamani kufunga ndoa na kuwa na familia lakini kutokana na kutokuwa na kazi nzuri pamoja na maisha yanayoridhisha anaogopa kuwa mazao ya ndoa hiyo hataweza kuyamudu.
Uchenna Udogu mwenye umri wa miaka 40, yeye amekaririwa kuwa alidai kuwa hataki kufunga ndoa kwakuwa hataki usumbufu kwenye maisha yake.
“Wote tunafahamu kinachotokea kati ya wana ndoa katika familia nyingi hasa pale ambapo baba hana fedha. Hakuna mwanaume timamu anayetaka kuingiza kichwa chake kwenye hali kama hiyo,” alisema Udogu.
Kutokana na hali hiyo, mwanasheria maarufu mwanamke jijini Lagos, Barrister Sherry Osakwe alieleza kuwa endapo Serikali ya nchi hiyo haitaongeza jitihada za kutoa ajira na kuongeza kipato cha wananchi wake, wataathiri ndoto za kijamii za wanawake wengi wenye umri zaidi ya miaka 35 na kupunguza idadi ya familia zenye maisha ya ndoa yenye afya.
Wataalam wa masuala ya uhusiano wameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, hali hiyo imesababishwa pia na mabadiliko makubwa ya maisha katika jamii, hususan kuanzishwa kwa mahusiano ya kimapenzi yasiyo rasmi yanayochukuliwa kama mahusiano rasmi katika jamii. Hivyo, hatua ya ndoa inapoteza maana kwa vijana wenye uelewa mdogo.
Uchumi usiwe kisingizio cha kuoa. Quran Takatifu, Surah 24, tunaahidiwa kuwa tukioa tutabarikiwa na hata vipato vyetu. “Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafukara Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua.”
Biblia Takatifu inasema katika Kitabu cha Wimbo Ulio Bora sura ya 8, mstari wa 6-7, Mungu anasisitiza kuwa penzi halinunuliwi kwahiyo kipato kisiwe kisingizio, na atakayejaribu kulinunua mwisho ataambulia dharau.
“Nipige kama mhuri moyoni mwako, naam, kama mhuri mikononi mwako.
Maana pendo lina nguvu kama kifo, wivu nao ni mkatili kama kaburi.
Mlipuko wake ni kama mlipuko wa moto, huwaka kama mwali wa moto.
Maji mengi hayawezi kamwe kulizima, mafuriko hayawezi kulizamisha.
Mtu akijaribu kununua pendo, akalitolea mali yake yote, atakachopata ni dharau tupu. (Wimbo Ulio Bora 8:6-7”