Sikukuu ya Wakulima inayofahamika kama Nane-Nane, husherekewa nchini kote ifikapo Agosti 8 kila mwaka, ikitayarishwa na kuratibiwa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika la Chama cha Kilimo Tanzania – TASO, na kuhusisha mtu mmoja mmoja, Wizara na Taasisi zinazojishughulika na kilimo.
Kwa miaka ya nyuma, sherehe hizi zilikuwa zikifanywa Julai 7, kila mwaka kwa kuzingatia mafanikio makubwa na changamoto zinazokabili Sekta ya Kilimo, inayowashirikisha wadau wote kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.
Maadhimisho haya husherehekewa katika ngazi ya kanda, ambapo kwa mwaka huu zinafanyika katika kanda ya nyanda za juu za kusini kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Kwa kanda ya Kaskazini, sherehe zinafanyika Arusha, wakati kanda ya Mashariki zilifanyika Morogoro na Kanda ya Ziwa, zilifanyika Mwanza, Viwanja vya Nyamhongolo na Kanda ya mwisho ni kusini, zilifanyika Ngongo katika Mkoa wa Lindi.
Maonesho ya Mwaka huu (2023), yalifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ambaye aliitaka Wizara ya Kilimo na Mifugo kuanza maandalizi ya kuchukua vijana wengine katika programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT).
Pia Dkt. Mpango akaziagiza Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi kuona namna bora ya kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili vijana wa JKT wanaojitolea, kupewa kipaumbele kushiriki katika programu hiyo.
Anasema, Wakulima wanatakiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili taifa liweze kujitosheleza kwa chakula na kupata fedha zaidi za kigeni kutokana na mazao mbalimbali na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa kuwapatia Maafisa Ugani vitendea kazi.
Aidha, anasisitiza taasisi za kifedha na mabenki hapa nchini kuendelea kushusha riba zaidi, ili kuwasaidia wakulima na wafugaji huku akiitaka Wizara ya Kilimo na Fedha kufikiria kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya kilimo utakaosaidia kushusha riba kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Lakini ripoti ya hali ya usalama wa chakula na lishe duniani – SOFI, ya hivi karibuni inaonesha zaidi ya watu milioni 122 wanakabiliwa na njaa duniani tangu mwaka 2019, kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo hali mbaya ya hewa pamoja na migogoro ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine hayo yapo kwenye ripoti.
Ripoti hii, inaeleza kuwa ingawa maendeleo yameonekana katika kupunguza njaa barani la Asia na Amerika ya Kusini, Afrika inasalia kuwa eneo lililoathiriwa zaidi ambapo mtu mmoja kati ya watano anakabiliwa, na kwa wastani njaa ipo katika kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa kimataifa.
Nilimsikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akizungumzia ripoti hiyo ya SOFI, yeye anasema “ingawa kuna miale ya matumaini katika baadhi ya mabara lakini kwa kwa ujumla, tunahitaji juhudi kubwa na za haraka za kimataifa ili kuokoa Malengo ya Maendeleo Endelevu.”
“Ni lazima tujenge uthabiti dhidi ya migogoro na mishtuko inayosababisha uhaba wa chakula kuanzia kwenye migogoro hadi kwenye hali ya hewa” anasema Katibu Mkuu Guterres.
Kwa upande wa njaa na utapiamlo, ripoti hiyo imeeleza kuwa uwezo wa watu kupata lishe bora umeshuka kote ulimwenguni kote, zaidi ya watu bilioni 3.1 sawa na asilimia 42 hawakuweza kumudu lishe bora mnamo 2021. Hii inawakilisha ongezeko la jumla la watu milioni 134 ikilinganishwa na 2019.
Watoto hususan walio chini ya miaka mitano ni waathirika wakubwa wa utapiamlo, huku watu wa vijijini wakiwa ni waathirika zaidi wa njaa ikilinganishwa na watu wa mijini, lakini nchi zinapaswa kujipanga kwa sera bora kwani idadi kubwa ya watu wanahamia mijini, na hivyo tatizo la njaa linaonekana kuongezeka hata mijini.
Bila shaka, kufikia lengo la Maendeleo Endelevu la kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030 kunaleta changamoto kubwa. Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 600 bado watakuwa wakikabiliwa na njaa ifikapo mwaka 2030.
Vichochezi vikuu vya uhaba wa chakula na utapiamlo vimekuwa jambo la kawaida na hivyo hakuna chaguo jingine isipokuwa kuongeza juhudi za kubadilisha mifumo ya chakula kwenye kilimo na kuwasidia Wakulima katika mahitaji yao, ili kufikia lengo hilo namba 2.
Na ili kukuza suala la uwepo wa uhakika wa wa chakula na lishe kwa ufanisi, ni lazima kuwe na uingiliaji kati wa sera na hatua zichukuliwe, yaani uwekezaji lazima uongozwe na uelewa wa kina wa uhusiano mtambuka na unaobadilika, kati ya mwendelezo wa vijijini na mijini na kuijali mifumo ya kilimo cha chakula.
Sababu hizi zinatosha kabisa kusema hali iliyopo humlazimu Mkulima kula Mbegu, kwani changamoto mbalimbali za mabadiliko ya Tabianchi, uchelewaji wa pembejeo, ruzuku na utozaji wa riba kubwa inayopigiwa kelele na Makamu wa Rais.
Haya ni kati ya mambo machache korofi yanayohitaji kuangaliwa kwa jicho la ziada kunusuru hali, na mwisho Mkulima ni lazima asaidiwe la sivyo tuteseka wote kwa kukosa chakula.
Nihitimishe kwa kusema tunaweza kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu, kutambua haki yetu ya chakula kwa wote na kutetea haki yetu ya mazingira safi, yenye afya na endelevu kwa sababu bado tuna wakati wa kutenda na wakati huo ni sasa, hatupaswi kuacha hili kwa wengine kulirekebisha, halafu jambo zuri ni kwamba wapo watu ambao wanapaswa kuchukua hatua nao ni viongozi wetu na wafanye hivyo leo.