Tanzania na Japan kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa – JICA, zimesaini mikataba mitatu ya mkopo wenye masharti nafuu na msaada, yenye thamani ya Yen Bilioni 10.15, sawa na Shilingi 174.9 Bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa pembejeo za Kilimo na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania – TAFICO.
Hayo yamebai ishea na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba na kuongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kitaongeza tija katika kilimo kwa kununua pembejeo ikiwemo mbolea, mbegu bora za kilimo zitakazo ongeza uzalishaji wa mazao ya kipaumbele ikiwemo mpunga, ngano na alizeti, na kuweka mifumo bora ya upatikanaji wa chakula na lishe.
Amesema, ” Mikoa itakayonufaika na mradi huo wa kuendeleza kilimo kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora, Songwe, Mbeya, Njombe, Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu na Katavi na kuhusu mradi wa kuendeleza sekta ya Uvuvi, shilingi bilioni 2.6 zilizotolewa na Japan kama msaada na zitatumika kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania – TAFICO, hii ni nyongeza ya fedha za msaada wa Yeni milioni 200 sawa na shilingi bilioni 3.5.”
Awali, Balozi wa Japan Nchini, Yashushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa JICA, Hitoshi Ara, walisema mkopo na msaada huo uliotolewa umelenga kukabiliana na uhaba wa chakula unaoikabili dunia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mazingira, vita vya Urusi na Ukraine na janga la Uviko-19.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe alisema fedha za msaada kutoka Japan zitatumika kununua meli kubwa ya uvuvi katika Bahari ya Hindi, kujenga miundombinu ya kuhifadhi samaki na vitendea kazi vingine vitakavyo tumika kuinua sekta ya uvuvi na kuiingizia Serikali fedha za kigeni.
Mradi huo, unaotekelezwa kwa kipndi cha mwaka mmoja unatarajia kuongeza ajira 20,000 na kuiingizia Serikali zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.