Serikali ya Tanzania imeendelea na jitihada za kuwarejesha Watanzania kutoka Jamhuri ya Sudan kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo kati ya kikosi cha Jeshi la Sudan na kikosi cha Msaada wa Jeshi yaliyoanza tarehe 15 Aprili, 2023.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,, Dkt. Stergomena Tax amesema kuwa zoezi la kuwarejesha watanzania waliopo nchini Sudan si jepesi kwani viwanja vya ndege hususan Khartoum ambako ndiko kwenye mapigano vimefungwa.

“Kufuatia siku tatu zilizotolewa za kusitisha mapigano (kati ya tarehe 21 – 23 Aprili 2023) tumeweza kuwasafirisha watanzania 200 (wanafunzi, watumishi wa Ubalozi, na raia wengine) kupitia mpaka wa Matema, Ethiopia kwa magari na wote wapo salama,” alisema Dkt. Tax.

Dkt. Tax ameongeza kuwa Watanzania hao watasafirishwa kwa ndege ya Shirika la ndege la ATCL kuja Tanzania. Ndege hiyo ipo tayari kuwachukuwa na kuwarejesha nyumbani.

Kwa upande mwingine, Dkt. Tax amemshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza zoezi hilo kwa ujasiri na bila kuchoka, hadi kufanikisha kufikia hatua hii.

Kadhalika, Dkt. Tax amezishukuru taasisi zilizoshirikiana na Wizara kwa kujituma na kufanikisha zoezi hilo. Taasisi hizo ni pamoja na; Ofisi ya Rais, Balozi za Tanzania nchini Sudan, Ethiopia na Misri na pia Shirika la ndege la ATCL.

Tukio hili limetuonyesha umuhimu wa Taifa kujitegemea ikiwa ni pamoja na kuwa na ndege zake. Hivyo tuunge mkono juhudi za Serikali za kuimarisha amani na usalama na kuleta maendeleo.

Pamoja na watanzania, serikali pia imesaidia kuwaondoa raia wa nchi za Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia, Kenya na Msumbiji vilevile nchi za Uganda na Saudi Arabia zimesaidia kuwaondoa raia wengine wa Tanzania huku Dkt. Tax akitoa wito kwa mataifa yote kuendelea kushirikiana na kusaidiana katika nyakati nyingine kama hizo.

DC Lulandala aahidi kuipa CPB ekari 200 za uwekezaji bure
Watatu Wydad AC kuivaa Simba SC Ijumaa