Jijini Dar es salaam kuna Barabara maarufu ikijulikana kwa jina la Shekilango, ambayo inanzia maungio ya Barabara ya Morogoro eneo la Nyumba za NHC, mkabala na Kiwanda cha Urafiki ikipitia Mitaa yote ya Sinza na kuishia Maungio ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kituo cha Bamaga.

Ni watanzania wachache wanaojua historia ya Barabara hiyo iliyopewa jina hilo maalum kwa ajili ya heshima ya Hussein Ramadhani Shekilango ambaye alikuwa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, akishughulika na mambo ya Utawala, wakati wa Uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Makamu wake, Aboud Jumbe.

Shekilango ni nani.

Hussein Ramadhan Shekilango, alichaguliwa na Wananchi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Jimbo la Korogwe Mjini lililopo Mkoani Tanga, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1975 akiachia nafasi yake ya zamani ya Meneja Mkuu wa Shirika la Usagishaji Nchini la National Milling Corporation – NMC.

Hussein Ramadhan Shekilango.

Katika mwaka huo ndipo alichaguliwa na Rais Nyerere kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Utawala) akiwa chini ya Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu, Rashid Mfaume Kawawa.

Mwaka 1977 yalifanyika Mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri Nchini, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kulinda Taifa, Edward Moringe Sokoine aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Kawawa na Shekilango akabaki katika nafasi yake.

Vita ya Kagera.

Baadaye mwaka 1979 vikatokea Vita vya Kagera, ndipo Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania vikafanikiwa kumng’oa Madarakani Dikteta Idd Amin Dada wa Uganda na kumkabidhi Nchi Yusufu Lule kama Rais wa mpito wa Taifa hilo Jirani ingawa hakudumu sana madarakani.

Juni, 1979 Lule aliondoshwa madarakani baada ya kutofautiana na Baraza la Ushauri la Taifa la Uganda juu ya uteuzi wa nafasi za Mawaziri na nafasi yake ikachukuliwa na Godfrey Binaisa kisha vuguvugu la vita vya Uganda na Tanzania lilipomalizika na hali ya Uganda kuwa ngumu, ndipo Hussein Shekilango aliagizwa na Rais Nyerere kwenda kuweka mambo sawa na kuisimamia Serikali mpya ya mpito ya Uganda chini ya Usaidizi wa Balozi Faraji Kilumanga kati ya Juni 1979.

Ajali ya Ndege.

Mei 11, 1980 Ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ, ilipata ajali na kuanguka katika Kijiji cha Engwiki Wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, Vijana wawili wa Kijiji cha Engwiki, Munderei Agerukai na Muserieki Njonjoloi ndio walikuwa mashuhuda wa kwanza wa ajali hiyo ya Ndege aina ya Casena 402 yenye uwezo wa kuchukua watu nane, iliyolipuka baada ya kugonga kilima cha Komoloniki mita 300 kutoka kilele chake.

Inadaia kuwa ndege hiyo ilikuwa ikiruka kati ya Mita 5000 na 7000 kutoka usawa wa Bahari ikielekea katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, ambapo Askari wa Chuo cha Uongozi wa Kijeshi Monduli na wananchi wa kijiji cha Engwiki walitumia saa tano kutafuta na kukusanya Miili ya abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo iliyopata ajali.

Mwisho wa Shekilango.

Miongoni mwa abiria waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na Hussein Ramadhan Shekilango, Balozi Faraji A. Kilumanga – Balozi wa Tanzania Nchini Uganda na msaidizi Mkuu wa Shekilango, Faraji Iddi Msechu, Koplo Petro Kalegi Magunda – Askari, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Private Stephen Mtawa – Askari, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Mallya – Askari, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Luoga – Askari, Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Msafara wa Maofisa hao wa Serikali na Jeshi ulikuwa ukitokea Kampala Uganda kwenda Arusha kwa ajili ya kukutana na Rais Nyerere aliyekuwa kwenye Ziara ya Kikazi Mkoani humo, huku ikikumbukwa kwamba mara baada ya Mapambano ya Vita vya Kagera na Vikosi vya Tanzania kufanikiwa kumng’oa Nduli Iddi Amin, kilipita kipindi cha mpito cha Utawala wa Yusuf Lule na Godfrey Binaisa ambacho kilishuhudia machafuko Makubwa nchini humo.

Lengo la kukutana na Rais Nyerere lilikuwa ni kwenda kumtaarifu juu ya hali ya Usalama ya Uganda baada Mfarakano kati ya Rais Binaisa na Generali David Oyite Ojok (aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Uganda), mfarakano ambao ulitoa dalili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Humo.

Hata hivyo, kuanguka kwa Ndege hiyo, ukawa ndio mwisho wa uhai wa Hussein Shekilango (Apumzike kwa Amani), ndipo Rais Nyerere akamtaja kuwa ni miongoni mwa mashujaa waliokufa vitani na akaitangaza SINZA ROAD ibadilishwe jina kuwa SHEKILANGO ROAD, kama sehemu ya kuenzi mchango wake kwa Taifa.

PSG yajipanga kuibomoa Real Madrid
Al-Arabi yamtwaa Marko Veratti wa PSG