Heldina Mwingira.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeingia katika  mapinduzi ya kidijitali yenye matumizi makubwa ya intaneti na teknolojia ya kidijitali. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania — TCRA, ripoti ya Juni 2023 inaeleza kiwango cha ukuaji wa usajili wa intaneti kwa asilimia 17 kwa mwaka ambapo mwaka 2018 kulikuwa na sajili 23,808,94 zilizoongezeka hadi kufikia 34,045,384 mwishoni mwa Juni 2023. 

Kutokana na uwepo wa mapinduzi hayo, kumepelekea wimbi la matukio ya ukatili dhidi ya Wanawake mitandaoni unaohusisha madhara ya kimwili, kingono, na kisaikolojia ukifanywa mtandaoni au kupitia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), ambao umeelekezewa kwa mwanamke. 

Ukatili huu, hutokea kwa namna tofauti tofauti kama vile ukatili wa kufichua taarifa za kibinafsi, kutukanwa au kutolewa maneno yasiyo na staha, matamshi ya chuki, unyanyasaji wa kingono kutuma picha bandia mitandaoni, kutuma picha za ngono na za kibinafsi bila idhini. 

Kundi kubwa la wanawake wanaoshiriki katika siasa, mara nyingi hukabiliwa na ukatili mtandaoni  kwa sababu tu wao ni wanawake ambao wako mtandaoni na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, umebaini kuwa,  asilimia 79 ya wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao wakati wa uchaguzi Mkuu wa 2020.

Utafiti huo, pia umeonesha kuwa, uchaguzi mkuu wa 2020 ulikuwa kama moja ya nyakati ambapo idadi kubwa ya wanawake katika siasa walikabiliwa na unyanyasaji wa mtandaoni, hasa wale wa nafasi za viti maalum 19 vya upinzani ambao walipewa majina na kudhalilishwa mtandaoni kwa muda mrefu.

Tukiwa tunaelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 mara nyingi ukatili wa namna hii hutokea, ili kuharibiana kisiasa na kupoteza au kupungua ujasiri kisiasa.

Ukatili wowote huleta matokeo mabaya kwa mtu mmoja mmoja au jamii kwa ujumla. Kwa kuwafanyia ukatili wanasiasa wanawake hupelekea: Changamoto za kisaikolojia, huweza kupelekea mhusika kupata msongo wa mawazo hivyo kusababisha kujiua au kupoteza mwelekeo katika maisha.  

Dar24 Media ilizungumza na Grace Bruno, ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani, uliopo kata ya Liwiti,  jijini Dar es salaam amesema, ‘Wanasiasa wanawake wengi wanapata msongo wa mawazo na sonona hivyo husababisha  hofu na kuvunjika moyo kushiriki kwenye ngazi za uongozi na maamuzi wakihofia kudhalilishwa na kutwezwa utu wao.  

Alisema hali hiyo hudhoofisha na kuharibu uwakilishi wa kisiasa na kwamba, Wanawake wengi kwa ngazi mbalimbali za uongozi baada ya kufanyiwa ukatili hupoteza ujasiri katika majukwaa ya kisiasa au pale inapobidi kutoa hoja zake za kisiasa za kusaidia jimbo, kata au jamii husika. 

Ripoti ya Tech Media Convergence 2021 inaonesha hatua ambazo zilizochukuliwa wanawake wanasiasa baada ya kufanyiwa ukatili mtandaoni asilimia 3.5% walitoa taarifa kwa mamlaka husika, 41.7% waliacha moja kwa moja kutumia mitandao ya kijamii, 34.9% walipumzika kwa muda kutumia mitandao ya kijamii, 2.6% walitafuta ushauri wa kisheria uliotumika. 

Mara nyingi  wanasiasa wanawake wanaathirika kutokana na ukatili wa mitandaoni  Neema Lugangira ambaye ni mbunge wa Tanzania na  mwanzilishi wa Taasisi ya Omuka Hub akiwa katika mkutano unaohusu masuala ya maendeleo na ujumuishi wa kidijitali ikiwemo kuhamasisha matumizi ya mtandao kwa wanawake katika siasa, alisema wana mikakati mbalimbali ili kuwawezesha wanawake kutobughudhiwa katika masuala yanayohusu siasa. 

“Tumekuwa na majadiliano mazuri ya namna gani tunaweza kuimarisha uwakilishi na ushiriki wa wanawake katika siasa za mtandaoni na tumekubalina tutaandaa kamati ambayo itaenda kudadavua suala hili ili tuje na mpango kazi ambao tutakapokwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wanawake wataweza kushiriki katika mitandao ya kijamii kunadi sera zao bila bughudha,” amesema.

TARI yawafikia Wakulima waathiriwa mafuriko Hanang’

Aidha ameongeza kuwa, anatambua uwepo wa kadhia wanayopitia wanawake wanasiasa katika mitandao hivyo wao kama wabunge wanawake wameamua kubeba ajenda hiyo kusemea wanawake katika siasa kwa sababu wanatambua umuhimu wa kushiriki katika mitandao

Japokuwa Ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni unashamiri, lakini zipo sheria mbalimbali zinazolinda na kuzuia ukatili wa kijinsia mitandaoni. Sheria mama ambayo ni Katiba yetu 1977 inazungumzia kila mtu anatakiwa aheshimiwe

16.-(1) Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi.Sheria ya Maudhui ya Mitandaoni (Online Content Regulation 2020)ambayo inakataza na kutoa adhabu kurusha maudhui ya udhalilishaji ikiwamo picha/video za utupu, lugha za udhalilishaji zinazokwenda kinyume na utamaduni wa Mtanzania. 

Sheria ya Kimakosa ya Mitandao 2015 (Cyber Crime Act) Kifungu cha 23 kinakataza na kupinga uonevu mtandaoni kuwa ni kosa kisharia kwa mtu yoyote kufanya uonevu wa aina yoyote kwa kutumia njia za kieleketroniki na kufanya hivyo ni kosa kisharia, yeyote atakayekutwa na kosa hili atatumikia kifungo, kisichozidi miaka 3 jela au zaidi, au kulipa faini isyopungua milioni tano (5) au vyote kwa pamoja. 

Sura ya 16 kanuni ya Adhabu Sheria Na. 47 ya 1954  135.-(1) Mtu yeyote ambaye kwa makusudi ya kusababisha shambulio la kijinsia la aibu kwa kutoa maneno au sauti, kuonyesha vitendo au kutoa maneno, au kuonyesha ishara yoyote ambayo itaonekana na mtu mwingine atakuwa ametenda kosa la shambulio la kijinsia na akipatikana na hatia atawajibika na kifungo kisichozidi miaka mitano au faini isiyozidi laki tatu au vyote viwili, kifungo na faini.

(2) Endapo kosa la shambulio la kijinsia chini ya kifungu hiki litamhusu mvulana au msichana wa umri wa chini ya miaka kumi na nane, haitakuwa kinga kumshitaki mvulana au msichana huyo aliridhia kitendo kilichosababisha shambulio la kijinsia. 

Jamii inashauriwa kufuata sheria zote zinazolinda na kuzuia ukatili wa kijinsia mitandaoni ili kuepuka kwa kutokuwafanyia ukatili wanawake mitandaoni kwa lengo la  kuwawezesha wanawake wasiogope kujihusisha katika masuala ya kisiasa.  

Imefika wakati sheria inabidi ifuate mkondo wake ili wanasiasa wanawake wapate nafasi na fursa ya kutumia mitandao kwa uhuru bila kuvunja sheria kwa sababu mitandao ina faida katika kuwapa fursa na kukua kisiasa.

Dar24 Media pia ilifanya mahojiano na aliyekuwa Mwenyekiti wa Siasa kata ya Kimanga na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Jiji la Dar es Salaam, Winifrida Nindi kuhusu namna gani tunaweza  kujiepusha na Ukatili mtandaoni dhidi ya wanawake ambapo amesema TCRA, inabidi ishirikiane na wadau mbalimbali  katika kuondoa ukatili wa namna hii. 

Pia ametoa rai kwa vyama vya siasa katika kuwa na mbinu chanya katika  kunadi sera zao na sio sio kuwafanyia wanasiasa wanawake ukatili kwa lengo la kuwashinda kisiasa akisema, ‘Vyama vya kisiasa vinahitaji kurekebisha tabia na mbinu zao za kampeni ili kuhakikisha kuwa vinazingatia muktadha wa kisheria, na pia kuunda kanuni za maadili za ndani.

Aidha, ameongeza kuwa kuna uhitaji wa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zishirikiane ili kuweza kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi  na baada ya uchaguzi. 

Mitandao ya kijamii ina manufaa kwa wanawake wanasiasa kibinafsi na hata kwa upande wa  kisiasa  inawapatia nafasi ya  kujipambanua kisiasa, kuwapatia umma mambo yanayoendelea kwenye sehemu husika kuonesha fursa na ufanywaji wa shughuli mbalimbali katika jamii. 

Pia hutoa njia ya kipekee na mpya kwa wanawake kufikia wapiga kura wao na yanahimiza ujenzi wa jamii na kuwapa wanawake vijana na wanaharakati nafasi ya kujenga Ripoti ya Tech Media Convergence 2021 inaonesha asilimia 90 wanasiasa wanawake  wamekubali kuwa mitandao inawasaidia kujipambanua kisiasa.

Young Africans hawataki maskhara
Declan Rice kubidhiwa mkoba Arsenal