Na Ghati
Usiku wa Jumamosi iliyopita, Tanzania ilirejea kwenye mstari wa historia ya muendelezo wa mashindano ya urimbwende ambayo hakika tangu mwaka 1967, yalipoanza yamekuwa yakikumbwa na misukosuko pamoja na ‘vituko’.
Tangu mwaka 1994 yaliporejeshwa tena baada ya kusitishwa kwa muda mrefu, yamekuwa na historia ya kupendwa na kukosolewa, na hata kufungiwa baada ya waandaaji kuboronga.
Lakini mwaka huu, wengi tulisema mapele yamemtoka mwenye makucha baada ya kukabidhiwa aliyekuwa Miss Tanzania, 1998, Basilla Mwanukuzi ambaye alicheza karata yake ya kwanza Jumamosi iliyopita akiwa na kampuni ya The Look, na kumvika taji Queen Elizabeth.
Binafsi, nimpongeze Basila, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya The Look kwa kile walichokionesha Jumamosi hii. Nawapa asilimia 80, na zile asilimia 20 nazitupa kwenye ukosoaji ambao baadi ya Watanzania ndiko tunakopenda zaidi. Kwa bahati mbaya sana, wengi badala ya kukosoa tumekuwa ‘tukizodoa na kuchekelea’.
Kama mmoja wa wadau wa mashindano haya, naomba nitoe alama hizi kwa kutoyasikia mengi ambayo yalikuwa mdudu mbaya kwenye mashindano haya kwa miaka kadhaa:
Kwanza, The Look wamejitahidi kuhakikisha kuwa heshima ya warimbwende imelindwa.
Hakuna ripoti za tetesi za rushwa za ngono, kujuana, kupanga washindi, kufungia zawadi kama ‘mbuzi kwenye gunia’, kumpa ushindi asiye na vigezo, kuwaingiza kambini wasichana ambao ni ‘bibi bomba’ n.k. Haya Basila Mwanukuzi kweli umeyashinda vyema.
Lakini, asimia 20 naziondoa kwa ukosoaji wa maandalizi ya tukio lenyewe. Kwanza wengi walioshuhudia usiku ule, walikosoa zaidi upande wa burudani na amsha-amsha ya shindano. Tukio lilikuwa limepoa sana, na pia liligubikwa na hotuba nyingi hali iliyowachosha wengi.
Pia, zawadi ya mshindi ambayo ndiyo iliyozua gumzo, imekuwa ikikosolewa zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Gari hilo aina ya Terios Kid ambalo Basilla amesikika akieleza kuwa amelinunua Sh. Milioni 15, limekosolewa vikali na baadhi ya watu akiwemo aliyekuwa muandaaji wa Miss Lake Zone, maarufu kama Jembe ni Jembe ambaye ni mmiliki wa Jembe FM ya jijini Mwanza.
Uamuzi wa Ndege kurusha jiwe hadharani kwenye dirisha la nyumba aliyokuwa anajenga yeye pia, yaani kama mshiriki wa mchakato wa uandaaji wa Miss Tanzania ulinishtua. Lakini saa chache zilizopita, Ndege alikuwa ameweka picha za warembo kutoka Lake Zone akiwatakia kila la kheri, ikimaanisha kuwa anaunga mkono kinachofanyika.
Ndege aliungana na Jaqueline Wolper, ambaye alimvaa moja kwa moja muandaaji wa shindano hili na kukosoa vikali zawadi ya gari. Alidai ni bora simu aina ya iPhone X kuliko gari hilo.
Lakini maandishi ya wawili hayo yalifikia hatua ya kuweka hadhari kuwa walikuwa wanakisasi dhidi ya kitendo cha Basilla kuikosoa vikali hadharani zawadi ya Miss Lake Zone ambayo aliita ‘Skrepa’.
“Jamani mimi sina tatizo na huyu dada aliyeandaa Miss Tanzania, ila tatizo ni kwamba aliwaandama sana waandaaji wa Miss Mwanza juu ya zawadi mpaka wakapelekwa kwenye uongozi wa Serikali na kuandika barua mpaka mashindano kutaka kusitishwa,” aliandika Wolper.
Muandaaji huyo wa Miss Tanzania – kipengele cha Miss Lake Zone, alikumbushia pia jinsi ambavyo Basilla alidai Wolper hana vigezo vya kuwa Jaji wa shindano hilo, namna alivyosafiri kwenda Mwanza na kusimamia zoezi la zawadi, hali iliyowafanya waandaaji hao kununua zawadi nyingine na kuachana na ile ya kwanza ambayo inadaiwa kuwa ni gari lililotumika.
Bosi wake, Basilla pia alizidiwa na kuamua kujibu kwenye Instagram akirusha makombora yake mazito kumjibu Ndege. Hapo alitoa siri ya ulipoanzia uhasimu wao, akimtuhumu Ndege kuwa ana hasira za kukataliwa kuandaa Miss Tanzania na badala yake alipewa yeye.
Ugomvi huu kuwekwa hadharani, ni pigo lingine kubwa zaidi la mashindano ya Miss Tanzania na la aina yake, tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Yaani tumerekebisha asilimia 80 ya makosa, lakini waandaaji wenyewe tumeikosea heshima Miss Tanzania, wameleta aibu nyingine.
Kama ni kweli tunajenga Miss Tanzania mpya, kulumbana hadharani, badala ya kukutana kufanya tathmini ya jinsi ambavyo mashindano haya yameanza, tunarusha mawe kwenye nyumba ya vioo tuliyojinadi kuijenga. Kulipizana visasi na kutoleana siri za ndani ni kuliabisha shindano lionekane kama sio la kistaarabu. Hawa wana taswira ya shindano zima.
Mnatutia aibu kama taifa kwa visasi na hasira zenu binafsi. Kumbukeni hili shindano lina jina ‘Tanzania’.
Bassila afanye nini:
Basilla, kwakuwa ndiye mwenye kibali cha kuandaa pia Miss Tanzania 2019 anapaswa kuhakikisha kuwa anakuwa na kitengo imara na kinachofanya kazi kweli cha Mahusiano ya Umma (Public Relations), awe na ‘communication strategy’ nzuri itakayotumiwa kwa uhakika na idara hiyo. Hii itaepusha yeye kama Mkurugenzi kujikuta anarushiana maneno na watu kwenye Instagram. Sio lazima ahojiwe yeye na vyombo vya habari, aweke msemaji ili kuepusha hasira hizo za moja kwa moja kwa waliokwishakwaruzana, yeye aseme inapobidi.
Nimependekeza hili kwakuwa nimeona kuwa anachangamoto ya kutokuwa na kifua cha kubeba ‘ukosoaji usio wa kistaarabu’ (Emotional Intelligence).
Achukue kwa mlengo chanya ukosoaji, na kwakutumia idara ya Mahusiano ya Umma na njia nyingine, wakae wayachuje mazuri wayachukue ili kuboresha, mengine ambayo hayajengi wayaweke kando.
Bassila na The Look yake, wanapaswa kuhakikisha kuwa wanalinda kwa gharama yoyote ‘heshima na taswira’ ya Miss Tanzania, kuanzia ngazi zote za mikoa na kanda. Wahakikishe kuna wasimamizi wake wazuri tangu yanapoanza mashindano haya kwa ngazi zote. Ahakikishe mawasiliano yanakuwa katika njia rasmi, hata kwenye mitandao ya kijamii ili kuondoa majibu ya hasira na kulifanya shindano kuonekana kuwa la malumbano.
Ashikilie msimamo wa kuwafuatilia waandaaji wa mikoani na kanda hata zaidi ya alivyofanya kwa waandaaji wa Mwanza – Lake Zone, lakini alinde staha ya ulimi wake anapotoa maoni huenda ndio chanzo cha kuwakwanza wengi.
Ulikuwa mwanzo mzuri mwaka huu, ilikuwa hatua nzuri ambao ni kama ujenzi wa Ghorofa jipya. Bassila aliachiwa gari likiwa kwenye mlima, gari lenyewe lilikuwa na hitilafu kubwa.
Kuliwasha gari hili lilokuwa limeshindikana na kulipigisha hatua hata moja kuupanda mlima bila kurudi nyuma ina maana kubwa sana na anapaswa kupongezwa na pia kukosolewa kwa kujenga sio ‘kuzodolewa’.
Lakini kushambuliana kwa waandaaji na wale wanaodai kuwa ni wadau wenye uchungu na mashindano haya ni kudanganyana. Ni kama ‘wazodoaji’ wanatudanganya wanachangia ujenzi wa ghorofa zuri la Miss Tanzania, kumbe wanatamani lijengwe ghorofa la tope. Tukosoane kwa staha bila chuki na visasi. Pia, Basilla na The Look, tupe majibu kwa staha bila chuki na visasi.
Lakini, yote kwa yote, kama wasemavyo waingereza You deserve a round of applause.
Shukurani na hongera za pekee pia kwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayoongozwa na Dkt. Harrison Mwakyembe. Kipekee pia tulipongeze Baraza la Sanaa Tanzania kwa kukupa ushirikiano uliotukuka.
BTW: Hongera Queen Elizabeth, Miss Tanzania 2018 ambaye kwa mara ya kwanza ndani ya miaka kadhaa, ushindi wako haujapata ukosoaji wa maana. Unastahili taji hilo muhimu, tutakupa na bendera ukatuwakilishe vyema huko duniani. Inshallah!
*Makala hii ni maoni ya mwandishi, sio maoni au msimamo wa kampuni.