Hatimaye rapa Cardi B ameamua kuweka wazi chanzo cha kutaka kutwangana makonde na hasimu wake Nicki Minaj wiki iliyopita, kwenye hafla ya wiki ya mitindo iliyofanyika jijini New York nchini Marekani.

Lakini kabla hatujakueleza alichosema, tukukumbushe hali ilivyokuwa na kusababisha rapa huyo wa kike kuumia usoni.

Ingawa kulikuwa na taarifa tofauti-tofauti za jinsi ambavyo tukio hilo lilikuwa na kusababisha Cardi kuvimba sehemu ya paji la uso, TMZ walikusanya taarifa kutoka kwa vyanzo vya kuaminika zaidi vilivyoshuhudia.

Imeripotiwa kuwa Cardi B akiwa kwenye tukio hilo aliibua mvutano na ugomvi katika kibaraza cha ghorofa ya pili ya jengo hilo, wakati Chritina Aguilera akiwa anatumbuiza.

TMZ wameeleza kuwa rapa huyo wa ‘Be Careful’ alisikika akisema kwa sauti ya juu “ngoja nikwambie kitu”, huku akielekea alipokuwa Nicki Minaj lakini alizuiwa kabla hajamfikia. Lengo la Cardi alidai anataka kumchamba Nicki kwa uongo aliokuwa anaeneza kuhusu yeye na mtoto wake.

Cardi ambaye sasa anajiita ‘The Empress’ aliamua kuvua viatu vyake na kumfurumushia Nicki lakini vyote havikumpata rapa huyo anayejiita ‘The Queen’.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Cardi alipata uvimbe usoni baada ya kupigwa kiwiko na mtu ambaye alikuwa karibu na meza ya Nicki Minaj.

Rapa huyo wa kike ambaye ni mama wa mtoto Kulture aliyempata na mumewe Offset, aliamua kufunguka kupitia Instagram chanzo cha kutaka kumvaa Nicki.

“Nimewahi kukwambia mimi mwenyewe mara moja, nilikwambia mara ya pili mimi mwenyewe, na kila wakati umekuwa unazingua kuhusu ombi langu rasmi! Lakini unapomtaja mtoto wangu, unapenda kuchagua kunizungumzia mimi kama mama, kuzungumzia uwezo wangu wa kumtunza binti yangu ndio hapo unazingua/unaharabu,” ni tafsiri isiyo rasmi ya alichoandika Cardi, kwa kuondoa maneno yenye ukakasi.

Nicki Minaj bado hajazungumzia tukio hilo na anaonekana kuendelea na maisha yake ya kawaida.

Makala: Waandaaji Miss Tanzania kushambuliana, aibu ya nani?
David Seaman amtaka Leno kustahamili