Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Isdory Mpango anatarajiwa kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Sabasaba Mkoani Njombe Aprili 2, 2022 huku kauli mbiu kwa mwaka 2022 “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa”.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 29, 2022 Jijini Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi, amefafanua kuwa pamoja na Kauli Mbiu hiyo, Mbio hizo zitaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa Lishe bora, Mapambano dhidi ya Rushwa, Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, Mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na Mapambano dhidi ya Malaria.

Naibu Waziri Katambi amefafanua kuwa, baada ya Uzinduzi huo, Vijana sita walioandaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, watakabidhiwa jukumu la kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Mikoa 31 na Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195. Ameongeza kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza shughuli za maendeleo.

“Mwenge ni jicho la Rais Samia Suluhu Hassan, katika maeneo ambayo kote ana vyombo, anatawala na anamifumo ya kiserikali, hilo ni jicho la ziada, kote unakopita unakagua shughuli za maendeleo na unamulika miradi kwa kuangalia fedha zimetumika kama zilivyo pangwa na kama haijatekelezwa ipasavyo hatua stahikli zinachukuliwa,” Amesema Naibu Waziri Katambi.

Amesema kuwa, Mwenge wa Uhuru na Mbio zake umeendelea kuwa muhimu kwa taifa kwa kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi za kisiasa, dini wala makabila. Aidha, amebainisha kuwa, Falsafa ya Mwenge wa Uhuru, ndio chimbuko la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964 na Azmio la Arusha la mwaka 1967.

Mwenge wa Uhuru ambao kwa mwaka huu utaanza Mbio zake Mkoani Njombe tarehe 02 Aprili, 2022 unatarajiwa kufikia Kilele chake Mkoani Kagera tarehe 14 Oktoba, 2022. Mwenge huo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961.

Nchi ya DRC rasmi mwanachama wa EAC
Harmonize aweka wazi kuachana na Briana