Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imetoa onyo kwa wamiliki wa baa na kumbi za starehe za usiku ambazo zipo katikati ya makazi ya watu ambazo zinapiga muziki kwa sauti ya juu sambamba na kuzifungia kwa kukiuka sheria na kusababisha kero kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na namna wanavyotekeleza suala hilo la uchafuzi wa mazingira unaofanywa na upigaji kelele katika vilabu vya usiku.
Amesema wamebaini wengi wao wana leseni ambazo haziwaruhusu kuendesha biashara ya usiku katika maeneo yao kutokana na kutokidhi vigezo ikiwa pamoja na kuwa na kumbi ambazo hazitoi kelele ya muziki nyakati za usiku.
“Zipo baa na klabu ambazo zinajinasibu kwa ni night club lakini hazina sifa hizo na zipo zimejengwa katikakati ya makazi ya watu na bado zinaendelea kupiga muziki kwa sauti ya juu hatutakubali kuona uchafuzi huu wa mazingira ukiendelea”amesema Macha.
Katika hatua nyingine Macha amesema serikali inaheshimu sana madhehebu ya dini lakini katika wilaya yake yapo baadhi ya makanisa yamejengwa katikakati ya makazi hali ambayo imekuwa ikisababisha malalamiko kwa baadhi ya wapangaji ambao sio waumini wa madhehebu hayo.
Alisema baadhi ya makanisa hayo yamekuwa yakifungua muziki wa sauti ya juu katika makanisa hayo nyakati za usiku na kusababisha usumbufu kwa watu wengine hususani wagonjwa.
“Kuna sehemu tumetembelea na kukuta vifaa vipo tu pekee na vikiendelea kupiga muziki tuu bila ya kuwepo kwa waumini wa madhehebu hayo katika nyumba hizo”,alisema Macha.
“Tunawashauri viongozi wa dini kujenga makanisa yao katika maeneo ambayo yametengwa na Halmashauri ili kuondoa migogoro kwa wananchi”,alisema.