Mchezaji kiraka wa Young Africans, Said Juma Makapu amesema mabadiliko ya makocha katika kikosi hicho yamekuwa yakimgusa kwa nyakati tofauti.
Makapu amekua hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans mara kwa mara, licha ya kuonesha uwezo mkubwa pindi anapopata nafasi ya kuchukua nafasi za wachezaji wengine, wanapopata majeraha.
Makapu ambaye amedumu kwa kipindi kirefu Young Africans, amesema katika kipindi chote alichokaa klabuni hapo, kocha Eymael ndio alionesha kumuamini kwa kiasi kikubwa, tofauti na makocha wengine aliowahi kufanyanao kazi.
“Miongoni mwa makocha ambao wamewahi kunipa nafasi ya kucheza zaidi ni Luc Eymael pengine alikuwa anavutiwa na uchezaji wangu au mahitaji ambayo alikuwa anayataka nilikuwa nafiti vizuri,” amesema Makapu na kuongezea;
“Ambavyo nilikuwa napambana na kushindana kati mazoezi au kwenye mechi pindi yupo Eymael ndio hivyo hivyo nafanya wakati huu au mwingine.
“Bado nina imani nitakuja kupata nafasi ya kucheza zaidi kwani nafanya kila ambacho anahitaji kocha tukiwa mazoezini, pia akinipa nafasi kwenye mechi nifanya ambavyo anahitaji,” alisema
Tangu ameondoka Eymael katika kikosi cha Young Africans wamepita makocha wanne, Zlatko Krmpotic, Cedric Kaze, Juma Mwambusi na Nabi Mohamed wote Makapu si chaguo lao la kwanza.