Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu amesema wakati serikali na Jamii ya kitanzania inaendelea kupambana na ugonjwa wa Corona lazima jamii iendelee kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa mengine ya hatarishi ukiwemo ugonjwa wa Ukimwi.
Ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa anazindua uwekaji wa makasha ya kusambazia kondomu maeneo ya watu na yenye mikusanyiko huku akifafanua takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka takribani watu 72 elfu wanaambukizwa maambukizi mapya ya ukimwi.
Aidha Waziri Ummy ameihasa jamii kuacha dhana potofu ya kumuona tu aliyebeba kondomu kumuhisi kuwa ni muhuni bali jamii ijifunze kujilinda na maambukizi yatokanayo na ngono zembe ambazo zimekua zikiharibu maisha ya baadhi ya watu.
Sambamba na hilo pia amewaagiza watendaji wa TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Vijana Tanzania (TAYOA) kuhakikisha wanasambaza makasha hayo na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI hadi maeneo ya Vijijini ambapo baadhi ya jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo.
Makasha hayo tayari yamefika kwenye halmashauri 169 kati ya halmashauri 184 kwa Tanzania bara hivyo wajitahidi kufikisha maeneo mengi zaidi kuokoa taifa.